HALMASHAURI KUU YA CCM TEMEKE YAPOKEA NA KULIZISHWA TAARIFA YA UTEKELEZAJI ILANI YA CCM YA MBUNGE KILAVE


Na Mwandishi Wetu

Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Temeke, imepokea na kupitisha kwa kishindo taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM jimbo la Temeke, iliyowasilishwa  na Mbunge Dorothy Kilave.

Akifungua mkutano huo Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa CCM Wilaya Temeke, Zena Mgaya, amesema baada ya kupata taarifa ya utekekelezaji wa Ilani hiyo ya Mwaka 2021/22, kutoka kwa mbunge huyo, Dorothy, ameipitia na kulizishwa nayo.

Zena amesema mambo mengi yaliowasilishwa katika taarifa hiyo  yana mchango mkubwa serikali pamoja Chama.

Pia Zena alimshukuru Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ambayo imekuwa mfano wa kuigwa nchini na nje ya nchi.

Amewataka viongozi kuendelea kumuunga mkono Rais Dk.Samia kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama na kutatua kero za wananchi.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Daniel Sayi amempongeza mbunge Kilave kwa kuendelea kutekeleza Ilani hiyo vyema kwa weledi na kuboresha huduma za kijamii.

Sayi amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza vyema uwekezaji katika Bandari ambao unatija kubwa kwa Watanzania, hivyo wanaendelea kumuunga mkono.

Aidha amewaagiza viongozi wa Chama kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani kwa kasi, kuwepo kwa mafanikio makubwa na kuziagiza kamati za siasa za kata kukagua na kusimamia utekelezaji  wa Ilani kwa kuondoa changamoto zilizopo.

Naye Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdalah Mtimika, amesema Manispaa hiyo inaendelea kufanya vyema katika utekelezaji wa Ilani kwani mapato yanaongezeka kila kukicha. 

Amesisitiza kwa viongozi kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na kusema kuwa katika kipindi hiki utekelezaji wa maendeleo unaofanyika kwa kasi kubwa kuliko kipindi kingine hivyo kuwanyima wapinzani hoja.

Mtimika amewataka viongozi na wanachama wa CCM kuendelea kuteleza Ilani kwa umoja na mshikamano kumsaidia Rais Dk.Samia, kuepuka migogoro inayorudisha maendeleo nyuma.

Amesema endapo wakitulia vizuri na kuwa na umoja watapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kwa kumpa kura za kishindo  Rais Dk.Samia.

Akihitimisha uwasilishaji wa taarifa hiyo, Mbunge wa jimbo hilo, Dorothy Kilave, amewashukuru viongozi wa CCM na Serikali wa wilaya hiyo kwa ushirikiano ambao wanampatia uliomwezesha kufikia mafanikio makubwa ya kutatua kero ya wananchi.

Kilave amesema amezipokea changamoto mbalimbali zilizowasilishwa katika mkutano huo hivi wanaendelea kuzifanyia kazi ikiwemo ujenzi wa sekondari katika kata ambazo hazijajengwa, barabara na madawati.

Amewataka wananchi kuendelea kumpa ushirikiano katika kuendelea kutatua kero mbalimbali za wananchi.