Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, amewata vijana kujiendeleza kitaaluma ili kitanua uwigo wa ajira.
Soraga ametoa wito huo wakati akizungumza katika Mahafali ya tisa ya Chuo cha Mafunzo ya Amali, mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B, Unguja.
Amesema hatua hiyo inaendana na mpango wa Serikali katika ukuaji wa sekta ya mafunzo ya Amali nchini ili kuhakikisha inatimiza ahadi ya kuzalisha ajira laki tatu hadi ifikapo mwaka 2025 ambapo vijana wengi wataondokana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Aidha Mhe Soraga amewataka wahitimu hao wa vyuo vya Amali kuwa na ushindani mkubwa wa kiajira na uzalishaji kwani kasi ya maendeleo duniani ni kubwa sana na inahitaji vijana watakaoweza kufanyakazi kwa bidii na weledi mkubwa.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dr Mwanahamis Adam amesema Serikali kupiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuviendeleza vyuo hivyo ikiwemo kuongeza fani tofauti na kuajiri walimu wengi zaidi ili kukidhi mahitaji na kuongeza kasi ya ufundishaji.
Sambamba na hayo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Mhandisi Abadala Mohammed Hambal, amesema Mamlaka inatoa fursa za fani kulingana na soko la ajira hivyo amewasihi wanafunzi kuyatekeleza kivitendo waliyofundishwa ili kujitangaza kwa lengo la kupata fursa katika maeneo mbali mbali ikiwemo mahotelini, viwandani na sehemu nyingine.
Akisoma risala ya Chuo hicho Mwalimu Juma Mohamed Kesi amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana na kujiepusha kujiingiza katika makundi maovu, sambamba na kumuomba mhe soraga kuyafikisha maombi yao sehemu husika kuongezewa madarasa pamoja na kupatiwa eneo la kitosha la kufanyia shughuli zao ili kuzalisha vijana bora zaidi
Jumla ya wanafunzi 105 wamekabidhia vyeti vyo vya kumalizia masomo katika chuo hicho katika fani mbali mbali ikiwemo umeme, ushoni, fundi seremala,Tehama na mafundi wa vifaa vya umeme.