BODI YA MNH YARIDHISHWA NA MIRADI YA MAENDELEO

Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili imeridhishwa na hatua mbalimbali zinazofanywa na uongozi wa MNH ili kuimarisha hali ya utoaji huduma hospitali hapo.

Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Ellen Mkondya baada ya kufanya ziara akiwa na Wajumbe wa Bodi hiyo na kukagua miradi mipya ya maendeleo inayotekelezwa hospitali hapo ikiwemo eneo la mapokezi, la Idara ya Magonjwa ya Dharura pamoja na jengo maalumu litakalotumika huduma ya upandikizaji mimba.

“Kwa kweli tumefarijika sana, tumeona maendeleo makubwa ambayo yanaendelea kwa kasi sana, kuanzia unapoingia lango kuu unaweza kupata maelezo kupitia maulizo na hata wanaoingia na magari kuna utaratibu mzuri wa jinsi ya kupata tiketi ya maegesho tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari” amesema Dkt. Mkondya

Amesema kuwa katika Idara ya Magonjwa ya Dharura  kuna mapokezi ya wagonjwa wanaoweza kutembea wenyewe lakini pia eneo la kupokelea wagonjwa ambao wanaletwa na magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) na kwamba kwa sasa eneo limeongezwa tofauti na awali ambapo lilikuwa finyu.

“Tumeona pia vyumba vya kuhudumia wagonjwa wa dharura vina vitanda vya kutosha na wagonjwa wote wanaofika wanapewa huduma ya kwanza (triage) na kuimarishwa afya zao kabla ya kupelekwa kwenye matibabu zaidi kama ni hapahapa MNH, MOI au JKCI, lakini pia tumefarijika kuona wataalamu na vifaa vya kutosha kukabiliana na dharura” amesema Dkt. Mkondya

Aidha amebainisha kuwa jengo la kutolea huduma za upandikizaji mimba (IVF Centre) lipo katika hatua za mwisho za matayarisho, mitambo ya maalumu ya kusaidia uanzishwaji wa huduma hizo imeshawasili na kwamba hivi karibuni MNH itaandika historia ya kuwa Hospitali ya kwanza ya umma kutoa huduma ya upandikizaji mimba kwa wananchi.

“Naamini kabla ya mwishoni mwa mwaka huu huduma hii itaanza kupatikana hapa, utapangwa utaratibu mzuri ili huduma iwe bora na sisi kama bodi tutasimamia na kushauri kwa kuwa tunaamini itakapotangazwa kuanza mahitaji yatakuwa makubwa kwa hiyo na sisi lazima tujitayarishe kama Hospitali ya Taifa” ameeleza Dkt. Mkondya.