Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka vijana hususani wanamichezo wote katika Jimbo lake kuitumia fursa ya michezo katika kuwaongezea kipato na kuimarisha afya zao.
Dkt. Tulia ameyasema hayo Agosti 12, 2023 wakati wa kuhitimisha Mashindano ya Tulia Trust Uyole Cup yaliyofanyika katika uwanja wa Mwawinji Jijini humo ambapo Mtoni FC imeibuka mshindi wa mashindano hayo kwa kuifunga 2-0 Mwakaleli FC.
Amesema kuwa miongoni mwa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020 ni pamoja na kuboresha sekta ya michezo na katika kutekeleza ahadi hiyo tayari kwa miaka minne mfululizo amekuwa akidhamini mashindano hayo kupitia taasisi yake ya Tulia Trust huku kila mwaka yakifanyiwa maboresho.
Moboresho hayo ni pamoja na kuongeza idadi ya timu shiriki kutoka 32 hadi 74 na zawadi kwa washindi kutoka Shilingi Milioni 3 kwa mshindi wa kwanza hadi Shilingi Milioni 5.
Katika hatua nyingine, Dkt. Tulia ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkakati wake wa kuuboresha Uwanja wa Sokoine uliopo Jijini humo ili kuwa wa kimataifa.