DKT. TULIA AWATAKA WANANCHI KUWAKATAA WAPINGA MAENDELEO


Mbunge wa Mbeya Mjini, pia ni Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wananchi kote nchini kunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yao kwa ajili ya kuwaletea maendeleo na kuwapuuza wale wote wanaowashawishi kuyapinga.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 5 Agosti, 2023 wakati akifanya mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Mwakibete Jijini humo kwa lengo la kuwaeleza mambo aliyoyafanya katika kipindi chake cha Uongozi katika Jiji hilo na yale yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita.

Akitolea mfano wa baadhi ya maendeleo yaliyofanywa katika Jiji hilo ni pamoja na kuwezesha ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami na zaidi kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa barabara kuu ya njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma KM 218 ambapo tayari Serikali imeshatenga Shilingi bilioni 218 na mchakato wa ujenzi umeanza.

Katika sekta ya maji, Dkt. Tulia amewaeleza Wananchi kwamba Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 119 kwa ajili ya kusambaza maji kupitia mradi wa mto Kiwira ambao utasaidia kumaliza changamoto hiyo kwa Jiji la Mbeya na Mkoa kwa ujumla.

Kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Dkt. Tulia amewatoa hofu Wananchi kuhusu wanaopotosha kwa makusudi wakidai kwamba imeuzwa na badala yake amewaeeleza kuwa kinachofanyika ni ushirikiano wa kibiashara ambao utawezesha nchi kuongeza mapato yake na kusaidia kuharakisha maendeleo yao.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde, amewataka Wananchi wa Jimbo la Mbeya kujivunia na kumuombea Dkt. Tulia ili aendelee kuwaletea maendeleo ambayo wameyakosa kwa miaka mingi kutokana na kuibadilisha siasa za Jiji hilo zilizokuwa za kiharakati zaidi na sasa amezifanya kuwa za kimaendeleo.