MAJALIWA: MFUKO WA WATU WENYE ULEMAVU HAUJAUNGANISHWA NA MIFUKO MINGINE

Waziri Kassim Majaliwa, amesema Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu haujaunganishwa na mifuko mingine ya makundi maalum kama ambavyo inadaiwa.

“Katika risala yenu mmeomba Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu usiunganishwe na mifuko mingine ili uweze kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa kwenye Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Nitumie fursa hii kuwafahamisha kuwa mfuko huo haujaunganishwa na mifuko mingine na kama mlivyosikia, mfuko huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali kwa watu wenye ulemavu,” amesema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo, wakati akifungua kongamano la siku moja la watu wenye ulemavu Dar es Salaam lililofanyika kwenye ukumbi wa JNICC, jijini humo.

Alikuwa akijibu hoja kuu ya kwenye risala ilisomwa na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Ernest Kimaya ambaye alitaka wapate majibu ya Serikali kuhusu hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Watu wenye Ulemavu kwani wanaona ukiunganishwa na mifuko mingine, utasababisha masuala yao yafunikwe na kundi lao halitanufaika ipasavyo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuainisha changamoto zitakazowakabili kwenye matumizi ya fedha hizo endapo hawatajipanga kwa vile wana makundi mengi ambayo inabidi yaainishwe ili kila kundi liweze kunufaika na mfuko huo.

“Watu wenye ulemavu mna makundi mengi mno kama walivyo wasanii. Kuna wasanii wa muziki wa bongo fleva, orchestra, muziki laini, wa kufoka foka, bongo movie, wachoraji na wachongaji. Na hapa nimeona huo mchanganyiko. Mwenyekiti inabidi mkae na kuainisha haya makundi ili muweze kunufaika,” amesema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mkwamo wanaoupata watu wenye ulemavu katika maombi ya kazi kupitia utaratibu wa kidijitali wa Sekretarieti ya Ajira, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua uwepo ya changamoto hiyo na tayari imeweka utaratibu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“Waombaji wanatakiwa wawasilishe maombi kupitia Vyama vya Watu wenye Ulemavu ili wapate usaidizi kwa kuwa ofisi hizo tayari zina miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Mkurugenzi wa Idara, Kitengo cha watu wenye ulemavu upo hapa, simamia utaratibu huu ili kila nafasi za kazi zinapotangazwa wapelekee taarifa Vyama vya Watu wenye Ulemavu ili wapate usaidizi kwa wale wenye sifa zinazolingana na nafasi za ajira zilizotangazwa. Wekeni utaratibu mzuri wa kuwafikia ili nao wanufaike na fursa hizo.”

Akifafanua kuhusu ombi lao la kutaka kuharakishwa kwa utaratibu mpya wa kutoa na kurejesha mikopo inayotolewa na Halmashauri, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Kitaifa iliyoundwa kuandaa utaratibu mpya wa usimamizi wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mfumo wa kibenki iko katika hatua za mwisho za maboresho ya taarifa yake. “Niwasihi sana mvute subira na pindi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI atakapotoa miongozo yake basi miongozo hii itagusa namna nzuri ya kurejesha mikopo hii.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Naibu Waziri (OWM - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi alisema Serikali imeanza kukusanya fedha za kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004.

“Sera hii ni ya mwaka 2004, ni takriban miaka 20 sasa. Tumeanza kutafuta fedha ili kuibadilisha sera hii badala ya kuboresha sheria kwa kutumia sera iliyopo. Ili upate sheria nzuri ni lazima uwe na sera nzuri. Tumedhamiria kwamba kutakuwa na ushirikishwaji wa makundi tofauti kulingana na ulemavu walionao kwa sababu kila kundi lina mahitaji tofauti.”

Amesema Serikali imetoa sh. milioni 35 kugharimia upatikanaji wa hati ya kiwanja katika eneo la Mtumba, jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga Ofisi za Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu. Vilevile, Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI inaendelea kuratibu upatikanaji wa ofisi za vyama vya watu wenye ulemavu kwenye Mikoa na Halmashauri zote nchini.

Naye Mwenyekiti wa Keysha Empowering Development Foundation (KEDEF) ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Walemavu), Khadija Shaban Taya alisema kongamano hilo ni la tatu na kwamba amekwishaandaa makongamano kama hayo kwenye mikoa ya Dodoma na Mwanza.

“Nia ya makongamano haya ni kuwaleta pamoja watu wenye ulemavu ili watoe maoni yao na kuelezea changamoto zinazowakabili. Pia, tutawapa elimu juu ya sheria ya manunuzi ambayo inataka asilimia 30 itengwe na Halmashauri zote ili zitumike kuendeleza shughuli za watu wenye ulemavu.”