WANANCHI WA MBEYA MSIINGIZWE KINGI NA WAPINZANI, WAMEPUYANGA: DKT. TULIA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wananchi hususani wa Jimbo lake wajihadhari na watu wenye nia ovu ya kutaka kuwagombanisha na Serikali  yao ili wasishiriki katika mipango ya maendeleo yao.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 15 Agosti, 2023 wakati wa  Mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Iyela iliyopo Jijini humo na kusisitiza kuwa wakati Serikali ikijidhatiti kuhakikisha inafikisha huduma bora kwa jamii, wapo baadhi ya watu kwa makusudi wanajitokeza kutaka kuzuia jitihada hizo.

Amesema kuwa katika Jimbo lake ipo miradi mingi ya kimkakati iliyofanyika na inayoendelea kufanyika kwa kasi ikiwa ni baada ya yeye kuwa Mbunge wa Jimbo hilo ikiwemo elimu, afya na miundombinu  ambayo Serikali inatumia fedha nyingi zinazokusanywa kupitia kodi zinazotokana na uwekezaji.

Ameongeza kwa kusema kuwa ili kufanikisha hayo yote ni lazima Serikali ifanye uwekezaji na kukusanya kodi kama ambavyo imeamua kuongeza wigo mpana wa mapato kupitia bandari ambayo itawezesha kupatikana kwa mapato mengi zaidi.

“Niwaombe ndugu zangu Wananchi, wakati Serikali yenu inapambana kuwaletea maendeleo haya yote kuna watu huko wanahangaika kufanya porojo za hovyo na mwisho wa siku wameishia kupuyanga. Hivyo msije kuingizwa kingi na watu hao kwamaana hawana hoja” Amesisitiza Dkt. Tulia.