BONNAH ATOA AGIZO WANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA SEGERE AMBAO HAWAJARIPOTI SHULENI WATAFUTWE WENDE SHULE



NA HERI SHAABAN( ILALA)

Mbunge wa Jimbo la Segerea Bonnah Kamoli, ametoa agizo kuwafatilia wanafunzi wote wa kidato cha kwanza ambao hawajafika shuleni kuanza elimu ya sekondari. 

Bonnah ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kawaida ya sekta ya Elimu, kuangalia maudhurio ya wanafunzi walioripoti shuleni na miundombinu ya sekta ya Elimu, ambapo alifanya ziara kata ya Bonyokwa, Liwiti  na Mnyamani. 

"Ziara yangu hii ya kawaida nimeanzia shule ya sekondari ya Bonyokwa nayo imepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza,   Sekondari ya Liwiti ni shule ya pili nimeona katika taarifa yenu inaeleza idadi ya wanafunzi 400 mpaka sasa hawajafika shuleni, naagiza Halmashauri ya jiji kufatilia kujua wanafunzi hao wapo wapi, waje kusoma na endapo hawapo wameenda wapi, wakati wamepangwa katika shule hii", amesema. 

Bonnah amesema Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, inatekeleza Ilani kwa vitendo katika sekta ya elimu imejenga shule za msingi na sekondari katika jimbo la segerea ili watoto wetu waweze kupata elimu  bora. 

Aidha Bonnah, ametembelea Shule ya Sekondari ya Bonyokwa kuangalia miundombinu ya shule hiyo ambapo amekuta changamoto ya kukosekana kwa  uzio wa shule hiyo na Photocopy Mashine kwa ajili ya kudurufu mitihani ya majaribio.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Liwiti, Daudi Ng'wandu, amesema wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopangwa katika shule hiyo ni 820, ambao wamefika shule mpaka sasa na kuchukua fomu ni 500 na ambao wameanza masomo ni wanafunzi 420,  wanafunzi 400 bado hawajaripoti katika shule hiyo.

Mkuu Daudi Ng'wandu amesema Shule ya Sekondari Liwiti, jengo la kwanza lilianza Juni 2022,  madarasa 20 na matundu ya vyoo 45 wanafunzi wanaosoma shule za jirani watarejea Liwiti 370 wa kidato cha kwanza.