MAKONDA AZINDUA WIKI YA MAADHIMISHO YA MIAKA 47 YA CCM, KAULI MBIU NI 'SHIRIKI UCHAGUZI KWA UADILIFU NA KAZI IENDELEE'



 Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Paul Makonda akizungumza na Wananchi wa Shinyanga Mjini amezindua rasmi maadhimisho ya sherehe za miaka 47 ya Kuzaliwa kwa CCM.

Akizungumza mbele ya kadamnasi, Mwenezi Makonda amesema tunapoadhimisha miaka 47 lazima tutafakari misingi ya waasisi ambao ni wazee wetu waliokubaliana kuunganisha TANU na ASP.

Makonda ameeleza kuwa kwenye Katiba ya CCM imeeleza shabaha na malengo ya waasisi kuunda Chama Cha Mapinduzi ambapo moja ya shabaha hizo ni kuhakikisha tunaupoteza unyonyaji na dhulma kwa wananchi tunaowaongoza na kwa misingi hiyo ndio maana tunaenda kutimizia miaka 47.

Pia, Makonda amesema kuendeleza shabaha zao ni kutekeleza Ilani yetu kwa vitendo na ndicho kitu kinachopelekea kuheshimika na sio mavazi yetu ya kijani na njano hivyo kuacha kufuata shabaha hizo jambo hilo halitakubalika hata kidogo...kuanzia Mwenyekiti wetu wa CCM Dkt. Samia, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu pamoja na Sekretarieti ya CCM Taifa hawatakubali hata mara moja.

Aidha, Mwenezi Makonda amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi ya kata zote nchi nzima kwa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, kuongeza wanachama, kupandisha bendera na kufanya shughuli zingine mbalimbali za kijamii.