Na HEMEDI MUNGA, Iramba
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Suleiman Mwenda, amewapongeza na kuwashukuru Madaktari Bingwa na Bobezi kwa kuendelea kuokoa maisha ya wananchi kwa kutoa huduma bora.
Pia amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini.
Mwenda ametoa pongezi hizo, wilayani humo wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa utoaji huduma bobezi kutoka kwa Madaktari Bingwa.
Huduma hizo zimetolewa leo katika Hospitali ya wilaya, iliyopo Kata ya Old Kiomboi mjini humo, ambapo Mwenda amesema wataalamu hao wanafanya kazi kubwa.
"Niwapongezeni ndugu zangu Madaktari Bingwa, kwa kweli nakosa maneno ya kuwaambia lakini niseme tu mnafanya kazi kubwa, mnastahiki pongezi, hongereni sana," amesema.
Mwenda amesema nchi nzima inayoa Madaktari Bingwa 2,469 ambao wamegawanyika katika maeneo 28 na hiyo baada ya serikali kuweka juhudi kuendelea kuzalisha mabingwa zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma, hivyo licha ya uchache wao wanafanya kazi kubwa.
Amesema Madaktari wote nchini wameendelea kutoa huduma na kuhabarisha umma kuhusu magonjwa anuai, hata ukiingia katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari utakuta habari za afya zikiwemo za Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Profesa Janabi ambae anafahamika.
"Leo hii ukingia katika mitandao ya kijamii unakuta ushauri wa kidaktari, hivyo watu wanaendelea kuelewa aina ya maisha wanayoishi ikiwemo ulaji wa vyakula ndio chanzo cha magonjwa mengi yanayoendelea kuisumbua jamii hivi sasa," amesema.
Mwenda amesema Janabi amekuwa akitoa elimu ya afya namna ambavyo watu wanavyokula na wanavyoishi ndio msingi wa magonjwa, hivyo ukiona watu wanapata elimu hii maana yake kuna mafanikio katika sekta hiyo.
Mwenda ameongeza kuwa Profesa Janabi, ambae kwa sasa licha yakua yeye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo lakini anavyochambua mambo ya chakula, watu wanaelewa, hivyo anastahili pongezi kwa sababu watu wanapata ujumbe na wanamuelewa.
Amebainisha kuwa watalam hao wamekua wakijitolea hata pale wanapoona mgonjwa anaugonjwa ambao unadaiwa kuwa hatari na unaweza kuwaweka kwenye hatari ya kuwaambukiza, lakini Madaktari hao husimama mstari wa mbele kwa lengo la kuhakikisha afya za wagonjwa zinaimarika.
"Kwa kweli ni jambo kubwa, mnastahiki pongezi, namimi niwapongeze Madaktari wote nchini kwa kujitoa kiasi hichi," amepongeza DC Mwenda.
Kwa upande wa Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Bungando, George Kanani, amempongeza na kumshukuru, Mwenda kwa sababu amekua chachu ya wao kufika katika hospitali hiyo kwa lengo la kusogeza huduma bora kwa wananchi.
"Niwahakikishie ndugu zangu wananchi zoezi hili ni endelevu, leo tunaanza na kila baada ya muda tutakua tunarudi, hivyo niwatoe wasiwasi.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Paul, amempongeza, mkuu wa Wilaya hiyo, Mwenda kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kujidhatiti kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia baada ya kuboresha miundombiunu ya hospitali hiyo.
Amesema mwaka moja hivi karibuni walipokea vifaatiba vyenye thamani ya sh. bilioni 1.4 kwa sasa wanao mtambo mkubwa wa kuzalisha hewa ya oxygen kwa lengo la kuendelea kuwafikishia wananchi huduma bora.
Paul amemuhakikishia mkuu huyo wa wilaya, kuwa wananchi watawaona wataalam hao bure huku akiamini kuwa huduma hizo zitapunguza gharama kwa sababu awali walitakiwa kuzifuata huduma hizo katika hospitali ya rufaa ya Mkoa, Makihungu na St.Gaspar.
Amesema huduma zinazotelewa ni Madaktari Bingwa wa magonjwa ya ndani (TIBA, Physician), Daktari Bingwa wa Upasuaji wa jumla (General Surgeon), Daktari Bingwa Upasuaji wa Sanifu (Plastic Surgeon), Daktari Bingwa wa Upasuaji wa mifupa (Orthopedic Surgeon), Daktari Bingwa macho, Madaktari bingwa wa magonjwa ya Wanawake na uzazi.