TAASISI ZA KIJAMII ZAPATIWA MSAADA WA DOLA 20,000 KUTOKA SHIRIKA LA NVEP KWA UFADHILI WA BARRICK

 


Na MWANDISHI WETU

JAMII zinazoishi katika mazingira magumu zimepatiwa msaada wa dola 20,000 kupitia Taasisi zisizo za serikali za Mwangaza na Maktaba ya Jamii Martha Onesmi kukabiliana na changamoto za afya na elimu.

Msaada huo umetokana na sehemu ya fedha zilizotolewa na Taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP), iliyoanzishwa na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, kusaidia makundi maalumu,  Wanawake, watoto na makundi yenye uhitaji yasiofaidika na ukuaji wa kiuchumi barani Afrika.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido, amesema kila robo ya mwaka, taasisi hiyo  imetoa misaada yenye tija na manufaa ya moja kwa moja kwenye jamii zenye uhitaji.

“Hadi sasa tumeshatoa msaada kwa zaidi ya mashirika 15 nchini Tanzania  kupitia Taasisi ya NVeP, lakini huu ni mwanzo, leo tuko hapa kuleta mabadiliko katika taasisi mbili kwa kuzipatia msaada wa dola za Kimarekani 10,000 kila moja,  kuboresha elimu, afya na lishe kwa watoto katika jamii ’’, amesema.

Kwa upande wa Mwanzilishi wa Maktaba ya Jamii ya Martha Onesmo, Jennifer Dickson, amesema  fedha hizo zitasaidia kuboresha huduma za maktaba hiyo kuwa za kisasa kwendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani kote.

Jennifer amesema Martha Onesmo ni maktaba ya kijamii iliyoanzishwa wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, mapema mwaka huu  kuwezesha jamii na wanafunzi wote kupata huduma za elimu.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwangaza (OMCW), Marshalo  Chikoleka,  amesema msaada  utasaidia kuboresha huduma kwa makundi mbalimbali yenye mahitaji ambayo taasisi hiyo inahudumia.

"Fedha hizi zinatasaidia kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia lishe bora, elimu na kuwezesha wanawake kiuchumi ”alisema Chikolela.

Chikolela alisema taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam, inajishughulisha na kuwezesha wanawake kiuchumi, elimu na afya ya mtoto katika jamii.