Na HEMEDI MUNGA, Iramba
MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda ameitikia wito wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango wa kutoa elimu kwa watanzania hususan vijana kwa lengo la kuhakikisha wanapata uwelewa wa kufahamu historia ya inchi ikiwemo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
DC Mwenda ameitikia wito huo kwa kutoa elimu kuhusu Muungano, uliyoambatana na zoezi la kupanda miti katika viwanja vya shule ya Sekondari Kinambeu wilayani hapa.
Akizungumza na wanafunzi hao baada ya kupanda miti, DC Mwenda amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano chini ya kauli mbiu isemayo: Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania "Tumeshikana na Tumeimarika, kwa Maendeleo ya Taifa." wameendelea kuhamasisha kutunza mazingira.
"Tunapanda miti kwa lengo la kuendelea kuonesha jamii ikiwemo nyinyi wanafunzi namna bora ya kutunza mazingira, hivyo leo tunapanda miti hii," amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wanafunzi hao na wa shule zote kuendelea kupanda miti kuzunguka eneo la mipaka ya shule zao.
Kwa upande wa Muhifadhi Misitu Ofisi ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania wa wilaya hiyo (TFS), Rehema Mwinyimkuu amesema wanaungana na Mkuu huyo wa wilaya kuadhimisha Muungano kwa kupanda miti maeneo mbalimbali.
Aidha, amesema wamefanikiwa katika wiki hii kugawa miti 3,000 katika shule mbalimbali huku zoezi hilo likiendelea.
"Nitoe wito tuitunze miti hii kwa faida yetu sisi na kwa vizazi vijavyo, misitu ni mali tulioirithi, hivyo tuwarithishe wengine", amesema.
Ameweka wazi kuwa wakati wanafunzi hao wanakuja shuleni walikuta miti imepandwa na watu wengine, hivyo na wao wapande miti kwa lengo la kuacha kumbukumbu na kutunza mazingira.
Pia, amesema hatua hiyo, itasaidia kuendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuendelea kuhakikisha rasilimali za misitu zinaendelea kupatikana katika mazingira yao.
Naye Makamu Mkuu wa shule hiyo, Fabians Leo, amemshukuru DC Mwenda kwa kuichagua shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zinazopata miti ya kupanda kwa lengo la kuendelea kutunza mazingira.
"Katika Maeneo yetu tumejitahidi kupanda miti kupitia Klabu yetu ya Mazingira," amesema.
Aidha, ameahidi kuendelea kupanda miti ikiwemo kuitunza miti inayopandwa.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusu Miaka 60 ya Muungano, mazungumzo yaliyofanyika katika Makazi ya Makamu wa Rais Jijini Dodoma.
Amesema ni muhimu vijana kujifunza kupitia nyaraka, vitabu na kutambua historia ya Muungano na namna serikali zilivyofanya utatuzi wa changamoto mbalimbali kuhakikisha Muungano unadumu.