Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, amesema kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ndiyo siri na chachu ya Chama na viongozi wake katika kuwatumikia wananchi.
Balozi Dk. Nchimbi amesema katika kutekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R ya Rais Samia na kuwatumikia wananchi waliokipatia dhamana ya kuongoza, CCM kikiwa Chama kiongozi nchini, kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja wenye mshikamano bila kubaguana kwa kuangalia maeneo wanayotoka, dini, kabila wala itikadi za kisiasa.
Balozi Dk. Nchimbi, ameyasema hayo wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha Burundi, CNDD – FDD, Révérien Ndikuriyo, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar Es Salaam, Ijumaa, Mei 3, 2024.
“Asante kwa pongezi zako za utekelezaji wa Ilani ya CCM, mojawapo ya nguzo za uimara wa CCM ni pamoja na kazi kubwa zilizofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka hii mitatu, zinatupatia ujasiri na jeuri ya kwenda barabarani kuzungumza na wananchi kwa sababu tunayo mambo ya kusema na kuonesha na wananchi wanatuunga mkono", amesema.
Pia amesema katika uhusiano kati yao CCM wanafurahi namna ambavyo Rais Dk. Samia na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye ni marafiki, hivyo vyama vyao ni marafiki, nchi zao ni rafiki na hata viongozi wao ni marafiki, ni wajibu wao kuendelea kuenzi na kulinda uhusiano na ujirani mwema, kwa watu wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Ndikuriyo amesema CCM na Tanzania kwa ujumla, ni sehemu muhimu kujifunza kwa ajili ya kujiimarisha, hususani wakati huu ambapo Chama cha CNDD – FDD kinaendelea kuisimamia Serikali ya Burundi katika kulinda misingi ya demokrasia inayotokana na utashi wa Warundi.
Katika ujumbe wake, Mhe. Ndikuriyo aliambatana na Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Leontine Nzeyimana na maofisa wengine wa Chama cha CNDD - FDD kutoka Burundi.