BALOZI DK. NCHIMBI: MFUMO WA ELIMU UTAWASAIDIA WATANZANIA KUSHINDANA KIMATAIFA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi, amesema mageuzi makubwa ya mfumo wa elimu ya Tanzania yanayofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan yataweka msingi imara wa mabadiliko yatakayowasaidia vijana wa Kitanzania kushindana duniani. 

Balozi Nchimbi amesema msingi huo kupitia elimu, pia utawasaidia vijana wa Kitanzania kumudu changamoto za kuwa raia wa ulimwengu ambao unazidi kuunganishwa na kuwekwa karibu au kuwa kitu kimoja kupitia changamoto au fursa mbalimbali, kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidiplomasia.

Katibu Mkuu Balozi Nchimbi amesema hayo alipowahutubia wanafunzi, wazazi na Jumuiya ya Shule ya Dar Es Salaam International Academy (DIA), alipokuwa mgeni rasmi wa mahafali ya wahitimu wa kidato cha sita wa shule hiyo, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, jijini Dar Es Salaam.

“Katika ulimwengu unaozidi kuunganishwa na masuala mbalimbali, ambapo tunakutana na jamii na tamaduni tofauti kila siku, elimu ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kutusaidia na kuwajengea msingi imara vijana wetu hasa wanapopambana kenye hii dhana ya raia wa kimataifa…ulimwengu umekuwa mahali padogo na kuzidi kutufanya sisi kuwa raia wa dunia katika nyanja tofauti tofauti. Tunapaswa kuwa sehemu ya washiriki washindani sio kujitenga.

“Chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inafanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu kuendana na mahitaji ya kimataifa, ili kuweka mkazo katika mahitaji ya nyakati za sasa na mbele zaidi ili vijana wetu washindane kimataifa. Maendeleo ya ulimwengu yametuonesha ukweli kuwa uraia wa nchi yoyote kwa sasa, hauwezi kuepuka kukamilishwa na uraia wa kimataifa, kwa maana ya kuelewa jinsi ulimwengu unavyofanya kazi, kuthamini utofauti, na kushirikiana kutafuta majawabu ya changamoto na kutumia fursa mbalimbali zilizopo kila mahali,” amesema Balozi Nchimbi.

Aidha, Balozi Nchimbi alisisitiza pamoja na Tanzania kuweka maandalizi ya msingi imara kwa ajili ya watu wake kuwa na uwezo wa kushindana kimataifa, kwa kupitia nyanja mbalimbali, pia imejidhatiti kuendelea kuenzi, kuthamini na kulinda mila, desturi na tamaduni ambazo zimekuwa tunu na utambulisho wa Tanzania na Watanzania katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo katika kushindania fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake.

Mbali na mahafali ya wanafunzi wa kidato cha sita, Shule ya DIA pia mwaka huu inasherehekea miaka 20 tangu ilipoanzishwa kuwa mojawapo ya taasisi zinazotoa elimu nchini, ikiwa imejikita katika mtaala wa IB (International Baccalaureate).