Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wa Serikali waondoe ukiritimba kwenye suala la upatikanaji wa habari ili kuwawezesha wanahabari kupata taarifa sahihi na kufanya kazi zao kwa ufanisi.
“Viongozi na Watendaji wa Serikali na Mashirika zingatieni Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya Mwaka 2016 na ondoeni ukiritimba katika suala la upatikanaji wa habari ili wanahabari wawezeshwe kupata taarifa sahihi na wafanye kazi zao kwa ufanisi wa hali ya juu,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Mei 3, 2024) wakati akizungumza na wanahabari na wadau wengine kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Kuhusu upatikanaji wa habari sahihi, Waziri Mkuu pia amewataka wakuu wa taasisi waweke mazingira mazuri kwa waandishi wa habari ili kuwawezesha kuzingatia weledi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa ngazi zote za jamii.
Aidha, amevitaka vyombo vya habari viunde madawati maalum yatakayoratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi. “Madawati hayo yatafute fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango wa mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu kuandika kitaalamu masuala ya mabadiliko ya tabianchi na madhara yake kwa jamii na Taifa. Suala hili likamilike ili katika maadhimisho ya siku hii mwakani, iwepo taarifa ya utekelezaji,” amesisitiza.
Kuhusu habari za uchunguzi, Waziri Mkuu amesema uandishi wa habari hizo unahitaji rasilimali fedha za kutosha ili kutoa mafunzo na kuifanya kazi yenyewe. “Niwaombe wadau wote muhimu wakiwemo taasisi, asasi za kiraia na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi washirikiane na vyombo vya habari katika kufanikisha utafiti na uandishi wa habari za uchunguzi na kuvisaidia vyombo vya habari kukua kitaaluma na kiuchumi.”
Akigusia changamoto zinazowakabili waandishi wa habari wanawake, Waziri Mkuu amezitaka Wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na ile ya Maendeleo ya Jamii Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, zihakikishe zinakamilisha awamu ya pili ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC II). “Hatua hiyo itasaidia ushughulikiaji wa changamoto za mashambulio ya kimwili kwa waandishi wa habari wanawake,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwahimiza wanahabari wote wazingatie uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi kwa kutoa mchango chanya kwa jamii kwani wasipofanya hivyo tasnia hiyo inaweza kuwa chanzo cha kufifisha maendeleo na hata kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema vyombo vya habari vinayo nafasi kubwa ya kuitangaza nchi pamoja na kuijengea taswira chanya kimataifa na kuwapomgeza wanahabari kwa kazi wanayoifanya ya kuuhabarisha umma.
“Vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha uwekezaji, kutangaza vivutio vya utalii na kuchangia katika kuinua uchumi wa Taifa letu. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wote wa Tanzania ninavipongeza sana vyombo vyetu ya habari kwa kazi kubwa inayofanywa katika kuutumikia umma.”
Akisisitiza umuhimu wa vyombo hivyo, Waziri Mkuu amesema vina mchango mkubwa wa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli na utekelezaji wa mipango ya Serikali pamoja na kampeni muhimu za kitaifa.
“Waandishi wa habari wana nguvu ya kuongeza sauti kwa jamii kuhusu mmomonyoko wa maadili, athari za kimazingira, kufichua rushwa na uzembe na kuunga mkono masuluhisho yatakayochochea maendeleo endelevu na ustahimilivu katika maeneo muhimu.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2024 inasema: “Uandishi wa Habari na Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi.”
Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini imeimarika ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
“Hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini inaendedelea kuimarika. Bado hatujafika tunakotaka kwenda lakini kwa hakika hatupo tulipokuwa jana. Tumefika hapa kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais, tumetekeleza 4R za Mheshimiwa Rais na ndiyo maana tuko hapa tulipo,” alisema.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo mabalozi wa Marekani, Uswisi, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, UNESCO, Asasi za Kiraia, Wawakilishi kutoka Muungano wa Klabu 28 za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Jukwaa la Wahariri na wanavyuo.