BABARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Mwanza, wametoa elimu ya matumizi sahihi ya zebaki kwa wachimbaji wa madini katika migodi ya Chata, Shokeraera, Shilalo na luhala iliyopo Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza,
Akitoa elimu hiyo iliyohusisha matumizi salama ya kemikali ya zebaki kwa wachimbaji hao , Meneja wa Usajili wa Kemikali na Maabara za Kemia kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Musa Kazumila, amesema elimu hiyo ni utekelezaji wa mkataba unaofahamika Minamata unaotaka kutekeleza matakwa yake ambapo moja likiwa ni kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo.
Kazumila amesema mradi huo wa utoaji elimu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kuratibiwa NEMC, Mkemia Mkuu amepewa jukumu la kutoa elimu ya usimamizi salama na matumizi sahihi ya zebaki kwani ndiye anayesimamia utekelezaji wa Sheria Namba 3 ya mwaka 2003 ya udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani ikiwemo zebaki.
Aidha amefafanua lengo la utoaji wa elimu hiyo ni kuwajengea uwezo wa uelewa wachimbaji hao wa madini na watumiaji wa zebaki kutambua jinsi zebaki inavyoingia mwilini, madhara yake namna ya kujikinga.
Naye Ofisa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma, Dereki Masako, ameainisha maeneo ambapo madhara ya zebaki yanatokea kuwa ni wakati wa usagaji wa mawe na kudondosha matope ili zebaki ikamate.
Pia amesema wakati wa uchukuaji wa kusanyiko ambapo mchimbaji anapokamua na kitambaa kwani matone hudondoka chini na kusambaa ardhini na hewani na kuleta madhara.
Masako, ameeleza ni vema wachimbaji kutumia vifaa kinga kujilinda dhidi ya athari za zebaki .
“Madhara ya zebaki ni kuharibu mfumo wa fahamu na kuleta athari ya kushindwa kuhisi, kukakamaa kwa mwili, macho kuharibika na huathiri figo”, amesema Masako.
Amesema zebaki huathiri ukuaji wa mtoto pindi sumu ya kemikali hiyo inapopita katika kondo la mama, kupoteza nguvu za kiume kwa wanaume, msongo wa mawazo na mwili kuwasha na kupungua.
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka Chama cha Wachimbaji Wadogo Wilaya ya Misungwi, walishukuru kwa kupata elimu hiyo juu ya matumizi sahihi ya zebaki kweni wengi hawakuwa na uelewa wa madhara ya kemikali hiyo inayotumiwa zaidi na wachimbaji wa madini yaa dhahabu.