Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa Wakunga na wataalamu wa afya nchini kufanya kazi kwa weledi na kuongeza bidii katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.
Amesema kada zote za afya zinasimamiwa na miiko na maadili ya taaluma na miongozo iliyowekwa. "Hivyo basi kila mmoja ahakikishe anazingatia maelekezo mahsusi ya utendaji wa kazi."
Ameyasema hayo Jumapili, 5 Mei, 2024, alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Mkunga Duniani na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakunga uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Majaliwa amesema Chama cha Wakunga kiwe mstari wa mbele katika kukemea baadhi ya Wakunga wanaofanya kazi kinyume na maadili ya taaluma zao.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu na mazingira ya kutolea huduma ikiwemo kujenga majengo mapya, kufanya ukarabati wa majengo ya zamani na kujenga nyumba za watumishi karibu na vituo vya kutolea huduma ili kuhakikisha watoa huduma wanapatikana wakati wote.
"Serikali imeweka juhudi kubwa katika kununua vifaa tiba, dawa, pamoja na magari ya kusafirisha wagonjwa ili kurahisisha rufaa kati ya vituo vya kutolea huduma na wakati inapotokea dharura."
Majaliwa amesema serikali imeimarisha mfumo mzima wa rufaa kwa kushirikiana na wadau unaojulikana kama M-Mama.
Aidha, amesema maboresho hayo yamezingatia sana sehemu za kutolea huduma za mama na mtoto na kuhakikisha kuwa wodi za watoto wachanga na wale wenye matatizo (Neonatal Intensive Care Units) zinajengwa kwenye hospitali za Mikoa,Wilaya na baadhi ya vituo vya afya.
"Maboresho hayo yamechangia kuimarika kwa ubora wa huduma za Afya kwa kuwa yamegusa moja kwa moja mazingira ya kazi ya Wakunga na watendaji wengine wa sekta ya afya", amesema.
Kwa Upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa zaidi ya asilimia 80.
"Tunashukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za afya, hususan huduma ya mama na mtoto, ambayo imetuwezesha kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80", amesema.
Ummy amesema serikali imeridhia maombi ya muda mrefu ya Chama cha Wakunga ya kutofautisha kada ya wauguzi na wakunga.
"Naomba nitoe taarifa kwako tumepokea maoni na ushauri wa wakunga hususan katika mafunzo ya wakunga ngazi za chini, tunayo changamoto tunaenda kuibadilisha ili tuanzishe stashahada ya Ukunga."
Awali, Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dkt. Beatrice Mwilike, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya sekta ya Afya ambayo yamewezesha Wataalam wa huduma za Afya kufanya kazi katika mazingira bora.