Na Mwandishi Wetu- MoHA, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amesisitiza watanzania kuendelea kudumisha amani sambamba na kutumia nyumba za ibada kuhamasisha na kutoa mafundisho ya dini yatakayo dumisha amani.
Masauni amesema hayo Novemba 29, 2024 wakati akifungua Msikiti wa Tawhid eneo la Coco Beach ( Zamani Msikiti wa Makuti), Dar es Salaam, ambapo amesema Tanzania ni Nchi ambayo watu wanavumiliana sana na ndiyo maana ni rahisi kukuta watu wenye dini tofauti wanaishi kwa upendo, mshikamano bila kubaguana wala kuchukiana.
Amesema utamaduni wa kuvumiliana umejengewa misingi imara na waasisi wa taifa letu " ndio maana unaweza kukuta nyumba ya ibada ya dini moja anatokea muumini wa dini nyingine kutoa mchango wa ujenzi ni suala linalofanya nchi yetu kuzidi kuwa na amani" alisema Waziri Masauni.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref Nahd amesema kukamilika kwa msikiti huo utasaidia waumini kutekeleza ibada ya swala tano kwa waislamu wanaokwenda katiks fukwe hizo kutembea na kupumzika.
Aidha ufunguzi huo pia umehudhuriwa na Balozi wa Qatar nchini, Fahad Rashid Al Marekhi, Balozi wa Uturuki nchini, Dkt. Mehment Gulluoglu, Masheikh na waumini wa dini ya Kislam.