Vijana wa miaka 19 hadi 24 waongoza kwa maambukizi ya ukimwi Kinondoni



VIJANA wenye umri wa miaka 19-24 wametajwa kuongoza kwa  kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi katika Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa  katika Maadhimisho  ya Siku ya Ukimwi Duniani, ambayo katika wilaya hiyo  yamefanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saady Mtambule, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo,  Walada Abdallah, alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha inakomesha maambukizi hayo  kuendana na dira ya taifa kufikia mwaka 2030.

Walda amesema, wilaya hiyo imejikita kikamifu katika kutoa elimu ya kujikinga  dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, kupunguza unyanyapaa, ubaguzi , ushauri nasaha, kupima kwa hiyari na  usambazaji kondom.

Awali akisoma taarifa ya hali ya maambukizi ya ukimwi kwa ujumla ,Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Peter  Nsanya, amesema jitihada kubwa zimefanyika ambapo maambukizi  ya virusi vya ukimwi wilayani humo yameshuka kutoka  asilimia 4.7 mwaka 2023 na kufikia 4.2 imwaka huu.

Amesema vijana wa rika la kubalehe  kuanzia umri wa miaka 19 hadi 24 ndiyo wanaoongoza  kwa asilimia 40 ya maambukizi yote na jitihada kubwa zinaendelea kufanyika kuhakikisha maambukizi hayo.