Na MWANDISHI WETU
Balozi Liberata Mulamula, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakina mbadala kimejipanga vyema kuongoza nchi wakati wote, hivyo ana imani kubwa kitaibuka na ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Balozi Mulamula ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia nafasi ya CCM kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatano kuwapigia kura wagombea wa Chama tawala kwani kazi zake zinaonekana kwa utekelezaji wa Ilani chini ya uongozi imara na mahiri wa Mhe. Rais wetu, Dk.Samia Suluhu Hassan.
"Tunavyoelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wananchi wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi bora watakao tuvusha vizuri katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya maendeleo na ustawi wa jamii nzima.
"Aidha napenda kuwahamasisha wanawake wenzangu kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wenye uwezo wakiwemo wanawake waliopitishwa kuwania nafasi mbali mbali," amesema.
Amesema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema maendeleo ya Taifa letu yanategemea ‘ Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora’, hivyo wananchi waichague CCM yenye siasa makini, kwani hakina mbadala kitashinda kwa kishindo.