Na MWANDISHI WETU
Tume ya Ushindani nchini (FCC) imezindua wiki ya ushindani kitaifa huku wakijipanga kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria ili kujiepusha na vitendo ambavyo vinarudisha nyuma ushindani na maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Jijini Dar es Salaam, katika akizindua wiki ya ushindani, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio, amesema katika kusherekea siku muhimu ya ushindani duniani inayoadhimishwa Disemba 5 kila mwaka ambapo watakutana na kufanya semina na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na kufanya vipindi vya kuelimisha umma kupitia kwenye runinga na redio ili watanzania waweze kuelimika na kunufaika na elimu itakayotolewa.
Amesema wadau wote watakaokutana nao watapewa elimu na kuwajulisha FCC inafanya nini,serikali yao inafanya nini katika kuhakikisha kwamba sera na sheria za ushindani zinaondoa hali yoyote inayoondoa usawa sokoni na kurudisha nyuma maendeleo ya ushindani nchini.
“Tunazindua leo shughuli yetu na kuanzia siku ya jumatatu tarehe 02 na 03 December tutafanya semina kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria ili kuwaeleza kwa kina kuhusu siku yetu hii tukijikita katika kauli mbiu yetu na siku ya tarehe 04 December tutatoa elimu kwa umma kupitia runinga na redio ambapo kilele cha maadhimisho yetu haya yatakua December 05 mwaka huu”.