Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Swala Solutions na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, wamekabidhi msaada wa nyumba ya kisasa ya waalimu kwa Shule ya Sekondari Motongo, wilayani Tarime.
Akizungumza katika hafla hiyo, jana, wilayani Tarime, Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye, amesema msaada huo utawapunguzia changamoto waalimu wa shule katika suala la makazi na kutekeleza majukumu yao wakati.
Amesema kampuni hizo zimekabidhi nyumba pacha, mbili kwa moja yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 120 katika shule hiyo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa mgodi huo.
Kegoye amezishukuru kampuni hizo kwa kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wa miundombinu ya elimu hapa nchini hususan katika shule hiyo.
"Tunawashukuru wadau wetu maendeleo Kampuni ya Barrick na Swala, kutuwezesha kutatua changamoto hii ya makazi kwa waalimu, pia Barrick imekuwa ikitusaidia sana kuziondoa changamoto za elimu katika eneo letu", amesema.
Naye Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, amesema kitendo kilichofanywa na Kampuni ya Swala Solutions, ni mfano wa kuigwa kwa watu wote.
“Huu ni ushirikiano mzuri na katika vikao vyetu tunahamasisha wakandarasi, wazabuni kutoa kidogo kwenye sehemu ya faida yao kurudisha kwa maendeleo ya jamii,” amesema Christopher.
Pia Christopher amesema mgodi wa Barrick una manufaa makubwa kwa jamii inayoizunguka eneo hilo ikiwemo, kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR).
Kwa upande wa Kaimu Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Swala Solutions, Roy Kimutai, ameishukuru serikali ya kijiji, Kata ya Matongo na Halmashauri ya Wilaya Tarime kwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Zabron Orege amesema nyumba waliyokabidhiwa imefanya idadi ya nyumba za walimu zilizokamilika shuleni hapo kufikia nne, kila moja ikiwa pacha.
Pia Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyamongo Contractors and Mine Company Ltd, Samwel Paul Bageni, ameipatia shule hiyo msaada wa kompyuta mbili.