DK. GWAJIMA AWAONYA WAMILIKI WA MAKAO YA WATOTO KUWATUMIA KUJIPATIA FEDHA

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, amewaonya wenye vituo vya kulea watoto, kuacha kuwatumia kupata fedha kinyume na malezi.

Dk. Gwajima ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wamiliki wa makao ya watoto Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa baadhi ya wamiliki wanatumia rasimali fedha na chakula vinavyopatikana  kwa manufaa yao bila kunufaisha watoto.

“Wapo wanaowapiga picha watoto au kuchukua video kwa kusambaza mitandaoni ambapo ni kinyume na sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 158 na adhabuu yake ni kifungo cha miezi sita au faini isiyopungua sh. 500,000 au vyote viwili pia utafutiwa leseni yako, amesema.

Amesema endapo mmiliki ameshindwa kuendesha makao kutokana na ukosefu wa fedha anatakiwa atoe taarifa kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kufuata utaratibu za kufunga makao hayo na kuhamisha watoto pamoja na kufuta leseni.

Dk. Gwajima amesema mmiliki wa makao anatakiwa kuwa na kamati za makao zenye jukumu kisheria la kusimamia maslahi ya watoto na kushauri kuhusu utolewaji huduma bora makaoni, kwa mujibu wa kifungu cha 134 (2) cha sheria ya mtoto ya mwaka namba 21 ya 2009.

Amesisitiza kwa baadhi ya wamiliki wa makao kuacha kuwapa vitisho maofisa ustawi wa jamii wanapotekeleza majukumu yao ya ufuatiliaji na ukaguzi wa utoaji wa huduma na uendeshaji wa makao.

“Nawaelekeza kuwaruhusu maafisa wa Ustawi wa Jamii kuingia makaoni na kufanya ukaguzi wakati wowote inapohitajika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria kifungu namba 136, kumzuia ni kosa kisheria na sdhabu yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja na faini ya sh. milioni mbili au vyote pamoja,” amesema.

Dk. Gwajima amesema baadhi ya makao wanadahili watoto bila kupitia kwa maofisa wa Ustawi wa Jamii wakati wa kuwapokea hali inayopelekea kuwepo kwa watoto wasiokuwa na sifa  za kulelewa katika makao jambo ambalo sio sawa.

Amesema kila mmiliki anatakiwa kuhakikisha mtoto anayelelewa makaoni ameandaliwa mpango wa huduma unaoainisha mpango wa kuondoka makaoni kwa mujibu wa kanuni ya makao ya watoto ya mwaka 2012.

Pia, amewataka baadhi ya wamiliki wa makao kuacha tabia ya kuwazuia watoto wasiondolewe makaoni  na kuwanyima fursa na haki ya kuwa na familia zao ambapo ndio sehemu salama kwa mtoto kulelewa, hivyo wamiliki wanatakiwa kushirikiana na maafisa ustawi kuwaandaa watoto kwa kuwaunganisha na familia zao.

“Kumekuwa na taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia, baadhi ya makao wanakalia kimya matukio hayo, mnapaswa kutoa taarifa kwa ustawi wa jamii au polisi na kuwajibika yanapotokea.

“Naelekeza Serikali za Mitaa  kupitia Wakurugenzi wa Halmashauri  kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii wanafanya ufuatiliaji na ukaguzi wa kila siku wa uendeshaji wa Makao wa watoto  yaweze kuendeshwa kwa kufuata mujibu wa sheria , kanuni na miongozi ya uanzishaji na uendeshaji wa Makao ya Watoto,” amesema.

Dk. Gwajima amesisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili ya Kitanzania katika malezi na makuzi ya watoto katika makoa, wahakikishe watoto wanazijua mila na desturi zizizo na madhara yoyote kimaadili na kuhakikisha watoto wanakuwa karibu na familia zao.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Makao Mkoa wa Dar es Salaam, Evance Tegete, amemshukuru Waziri Dk. Gwajima kwa kuungana nao na kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kufuata maelezo aliyotoa.

“Kwa sisi mkoa wa Dar es Salaam tulishaandaa katiba ambayo itatuongoza na kufikia Desemba tutakuwa tumeanza kuitumia,” amesema.