Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amevunja uongozi wa Soko la Mabibo na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina .
Ametoa maagizo hayo, alipofika katika soko hilo kutatua mgogoro baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na uongozi wa soko.
Chalamila amekemea watu wachache katika soko hilo kukwamisha jitihada za serikali za kuliboresha na kuonya wasijaribu kumchezea.
"Tena msije mkanichokonoa na nikafunga soko hili hata leo. Hakuna hata mmoja atakayefanya chochote wala kunyanyua kichwa chake," amesema Chalamila.
"Inawezekana hamjanifahamu vizuri. Haiwezekani watumishi wa serikali wanakuja katika soko hili halafu mpumbavu mmoja anasimama kuanza kuzuia, mnaakili nyie au hamkufunzwa adabu?"
Pia ameeleza kuchukizwa na baadhi ya watu katika soko hilo kumzomea Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, kutishia kuchoma moto gari la Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo lililofika katika sokoni hapo kuzoa taka na kumzuia mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuanza ukarabati wa soko.
" Kuanzia leo nimevunja uongozi wa soko hili. RPC, TAKUKURU, waliofanya mambo hayo leo wasakwe.Wahojiwe.Hatuwezi kulea ujinga"amesema.
Amesema Rais DK. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa sh. milioni 600 kuboresha soko hilo linalolalamikiwa kuwa na changamoto nyingi.
Chalamila amesema uongozi uliokuwepo ulikuwa ukikusanya fedha nyingi lakini zilikuwa zikiishia katika matumbo ya watu wachache ambapo kiasi cha sh. milioni 49 hazijulikani zilipo.
"Narudia tena mkome kwelikweli na hakuna anayeweza kupanda katika hili kwa chwa. Nahapa ningeweza kuja peke yangu. Nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Mwanza, Kagera hakuna hata mmoja wa kupanda katika kipara hiki,"alibainisha Chalamila.
Amesema baada ya ukarabati mkubwa kufanyika wafanyabiashara wote walipo waendelee kufanya biashara bila kuongeza ushuru.
“Nilipanga makubwa hapa mnabahati kwelikweli. Serikali imeamua kwamba serikali itakusanya mapato na kufanya maboresho hivho ndiyo Rais Dk. Samia anataka,”ameeleza.
Aidha Chalamila amemuagiza Mkuu wa Wilaya na Halmashauri ya Ubungo, kuanza kazi mara moja katika eneo hilo ukiwemo ukusanyaji wa mapato na ukarabati wa soko.
“Hizi pesa za hapa ni za moto nikama maji ya betri. Mkisha kula mkashiba mistake kutusumbua. Wafanyabiashara wanataka waboreshewe miundombinu lakini watu wachache wanakula,”ameeleza.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashim Komba, amesema soko hilo linauwezo wa kukusanya zaidi ya sh. bilioni 1 lakini hivi sasa linakusanya sh. milioni 500 tu.
Amesema licha ya Rais Dk. Samia kutoa kiasi cha sh. milioni 600 kukarabati soko hilo lakini kikundi kidogo cha wafanyabiashara wa soko hilo kilifukuza mafundi, kutishia kulichoma moto gari la taka la Halmashauri ya Ungo na kuandaa mikakati ya kumzomea (mkuu huyo wa wilaya).
Amesema eneo hilo ni la Kiwanda cha Urafiki na tangu uongozi wa soko ulipochukua madaraka haujawahi kuoa gawio kwa kiwanda hicho na halmashauri hiyo.
Baada ya uamuzi huo wafanyabiashara waliserebuka na mkuu wa mkoa huyo kwa fulaha, kumbemba juu juu Mkuu wa Wilaya wakimwimbia nyimbo za ushushajaa.