Na Gregory Millanzi, Mtwara
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, amewasili mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku 4, kuanzia tarehe 14 mpaka 17 septemba 2023, ambapo atakagua miradi mbalimbali ya Maendeleo.
RaisDk. Samia amewasili jioni ya leo na kupokelewa na umati wa wananchi waliojitokeza kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara na kulakiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Ahmed Abasi na viongozi mbalimbali wa serikali.
Baada ya kushuka kwenye ndege Rais Samia amezungumza na wananchi na kuwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na amewaomba kujitokeza kwenye maeneo mbalimbali ambapo ataenda kutembelea miradi ya maendeleo.
Ratiba iliyotolewa na uongozi wa Mkoa wa Mtwara, Rais anatarajiwa kuanza kuzungumza na Wazee wa mkoa huo katika Ikulu ndogo, iliyopo Shangani septemba 14, 2023 baada ya kuwasili.
Ziara yake ya ukaguzi na uzinduzi wa miradi itaanzia Septemba 15, ambapo Rais Samia atazindua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, iliyogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 15.8 na kuhudumia wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, na kisha kukagua maboresho ya ujenzi wa Uwanja wa ndege ambayo yanaendelea unaogharimu shilingi bilioni 55.2.
Baada ya zoezi hilo Rais atakwenda kuzindua Barabara ya Mtwara-Mnivata, yenye urefu wa kilometa 50 katika eneo la Naliendele Manispaaa ya Mtwara Mikindani.
Hata hivyo anatarajiwa kuona na kukagua shughuli za uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Mtwara uliogharimu Shilingi Bilioni 157.8, na kuzungumza na hadhara ya wakazi wa Mtwara mjini katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.