Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha wahandisi wazawa wanashiriki kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali nchini.
Amesema kuwa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Tanzania, unaolenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka 9% hadi 8% ifikapo 2025/26, Serikali inatarajia kutimiza azma yake ya kuhakikisha inazingatia ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya ujenzi ili kukuza ujuzi.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi Septemba 14, 2023) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya siku wahandisi, katika ukumbi wa Mlimani city, Dar es Salaam.
“Wizara ya Ujenzi pamoja na bodi ya wahandisi inalifanyia kazi suala la ushiriki mdogo wa wazawa katika miradi ya maendeleo, hii ni changamoto ambayo mmeiibua, Serikali sasa imeliweka kwenye mpango wa kuhakikisha changamoto inafanyiwa kazi ili kuongeza idadi ya wazawa kushiriki katika kazi za ndani”
Amesema kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha wahandisi wazawa wananufaika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali “miradi hii ni fursa kwenu, natoa rai mjipange na kufanya juhudi za makusudi kila mmoja kwenye eneo lake ahakikishe kwa uzalendo alionao na mapenzi kwa nchi yake kuwa kinara katika sekta unayosimamia ili kulijenga taifa letu”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi iandae mpango mahsusi wa kuwaendeleza wahandisi wanawake ili waweze kusajiliwa kwa wingi zaidi wanapohitimu masomo “Suala hili litekelezwe kwa ushirikiano na wadau wengine wa uhandisi”
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenye amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa taaluma ya uhandisi katika sekta mbalimbali za kiuchumi kupitia uanzishaji wa viwanda, uendelezaji wa miundombinu ya kilimo, nishati, maji, uvuvi, utumiaji mzuri wa rasilimali na malighafi, usafiri na mawasiliano
“Katika mwaka 2023/2024 Serikali imetenga miradi maalum ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa ajili ya wakandarasi wanawake, ambao zabuni zitashindanishwa kwa makandarasi wanawake tu”
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Mhandisi Menye David Manga Amesema kuwa bodi inatarajia kufanya mageuzi makubwa ya teknolojia ili kuhakikisha wahandisi waliosajiliwa na wenye sifa wanakuwepo wa kutosha kwa ajili miradi mbalimbali nchini ili kujenga dhana halisi ya ushirikishwaji wa wazawa ‘local content’ “Tutakuwa na mageuzi katika sheria na kanuni zetu ili kuongeza usajili wa wahandisi”.