HAKUTAKUWA NA UCHAGUZI MDOGO KIGAMBONI - DK.NDUGULILE

Na MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile amesema hakutakuwa na uchaguzi mdogo  katika Jimbo la hilo lililopo Wilaya ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam, kwani yeye atamaliza muda wake, Mwezi Februari na uchaguzi utafanyika Mwezi October Mwakani.

Pia, alimshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kibali na kumwombea kura kwa viongozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika, kumuunga mkono apate nafasi hiyo, huku akiwapongeza mabalozi wa Tanzania nje ya nchi waliofanikisha ushindi huo.

Dk.Ndugulile aliyasema hayo, juzi, alipokuwa akikaribishwa wilayani humo na Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), Kanda ya Afrika.

"Nimepata simu nyingi, watu wakiuliza, lakini niwaambie Kigamboni hakutakuwa na uchaguzi mdogo wa jimbo, hakutakuwa na uchaguzi mdogo, Mimi nitamaliza Ubunge wangu Mwezi Februari Mwakani, ambapo ndiyo kipindi cha kudhibitishwa baada ya miezi sita, kwa mujibu wa utaratibu wa WHO.

"Hakutakuwa na uchaguzi mdogo hadi Mwezi Oktoba, utakapofanyika Uchaguzi wa Madiwani, wabunge na Rais," alisisitiza.