Na Mwandishi Wetu
Daktari wa Hospitali ya Kairuki ya Mikocheni, Fredy Rutachunzibwa, ameelezea namna teknolojia mpya inavyotumika kutoa matibabu ya kuondoa uvimbe mwilini bila kufanya upasuaji.
Mtambo unaotumika kuondoa uvimbe bila upasuaji unaoitwa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), tayari umeshaanza kufanyakazi katika hospitali hiyo kuanzia mwezi huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Dk. Rutachunzibwa ambaye alipata mafunzo hayo nchini nchini China, amesema mtambo huo tiba unatibu vimbe mbalimbali kwa kutumia mwangwi wa Ultrasound .
Amesema teknolojia hiyo ni ngeni katika nchi za Afrika, haitumiii mionzi kama ambavyo imezoeleka katika tiba l zinazohusiana na masuala ya uvimbe.
“Huu mtambo tiba unatibu vimbe mbalimbali mtambo hautumii mionzi kinachofanyika ni kwamba yale mawimbi sauti yanabadilishwa kwenda kwenye mfumo wa heat energy yanakwenda kuchoma sehemu yenye uvimbe tu bila kuathiri maeneo ya jirani yanayozunguka uvimbe huo,” amesema.
“Mfano kama uvimbe uko kwenye kizazi inamaana mayai hayatahusika kwenye tiba hiyo ni uvimve tu ambao utachomwa bila kuathiri maeneo ya jirani na kama ni kwenye titi tu basi kutachomwa kwenye uvimbe lakini sehemu zingine hazitaathirika kinachoathirika ni uvimbe tu,” amesema
“Tukishauchoma uvimbe tuna uwezo wa kuangalia hapo hapo je tumefanikiwa kwa kiasi gani na kama kutaonekana bado kuna kitu cha kurudia tutarudia lakini baada ya muda mfupi uvimbe unaanza kupungua na utapungua hadi utaisha kabisa na mhusika ataendelea na maisha yake kama kawaida,” amesema.
Aidha, Dk. Rutachunzibwa noamesema kwa mgonjwa ambaye amefanyiwa tiba hiyo wanatarajia ndani ya siku nne au tano uvimbe utaaanza kuisha taratibu kwasababu baada ya kuuchoma mwili unakuwa na kazi ya kuvunja vunja vile vilivyokuwa kwenye uvimbe na kuviondoa nje ya mwili kama takataka.
Amesema wanapomaliza tiba wanaendelea kumfuatilia mgonjwa kila baada ya miezi mitatu ili kuangalia mwenendo wa kupungua na hatimaye kumalizika kabisa kwa uvimbe.
Amesema maandalizi ya kumwingiza mgonjwa kwenye mtambo huo kwaajili ya kuanza matibabu hayo ni pamoja na kumtaka mhusika asile chakula chochote ndani ya saa nane kabla ya kuingizwa kwenye mtambo.
Rutachunzibwa amesema mgonjwa anapokuja kutaka kuondolewa uvimbe wanampima upya kwa vipimo vya Ultrasound, MRI na CT Scan vya hospitalini hapo ili kujiridhisha na aina ya uvimbe wanaotaka kuutibu.
“Lazima tuangalie kwanza tunatibu uvimbe wa aina gani, je ni uvimbe unaosambaa au uvimbe ambao hausambai, kama ni ule ambao hausambai lazima mtaaalamu achukue sehemu ya nyama akapime tuthibitishe kama ni uvimbe ambao hausambai,” amesema.
“Hata kama tukibaini uvimbe huo unasambaa unatibika kulingana na hatua aliyofikia mgonjwa, mfano ikionekana mhusika ana saratani ya ziwa lazima tujue uvimbe huo umeshasambaa au bado na ikitokea haujasambaa inawezekana kuutibu na ukaondoka kabisa,” amesema.
Pia amesema faida za tiba kwa kutumia mtambo huo ni kwamba mgonjwa hapati maumivu makali, anapata nafuu haraka, hapotezi damu na anaepukana na makovu ya upasuaji.
Amesema mtambo huo ni wanne kwa Afrika, ambao upo nchini Misri, Afrika Kusini, Nigeria na Tanzania katika hospitali hiyo.