MKENDA AZINDUA MAKTABA JAMII




Na Mwandishi Wetu


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema maktaba ya kijamii iliyoanzishwa na Mtanzania anayesoma Chuo Kikuu nchini Rwanda, Jennifer Dickson, itawasaidia vijana wengi kujisomea.


Mkenda alisema hayo, jana, katika uzinduzi wa maktaba inayojulikana kwa jina la Martha Onesmo, wilayani Mwanga, nakwamba maono ya Jennifer ya kuanzisha makata hiyo yatachangia maendeleo wa wananchi.

“Maktaba hii imekuja wakati muafaka ambapo Serikali imekuja na mabadiliko ya mfumo wa elimu yenye lengo la kuboresha elimu ya Watanzania, kwasababu maktaba itatumiwa na wanafunzi, walimu na wakazi wengine kujiongezea maarifa", alisema.

Alisema ya maono ya mwanzilishi wa maktaba hiyo yamewapa matumaini serikali kuwa mustakabali wa maendeleo ya nchi ni salama kwa sababu ina vijana wabunifu.

Mkenda alisema atahakikisha serikali itafanya kila linalowezekana maktaba hiyo inakuwa endelevu na inatunzwa.

Pia alisema serikali imeanza kutekeleza mpango unaolenga kuboresha maktaba zote nchini, kutoa fursa kwa wanafunzi, walimu na wakazi wengine wa ndani na wanaoishi nje ya nchi kupata ujuzi wa ziada.

Alisema serikali tayari imetenga takribani shilingi bilioni 2 kutekeleza mpango huo, ambapo maktaba 22 katika maeneo mbalimbali nchini zitaboreshwa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maarifa zaidi kupitia maktaba hizo.

Kwa upande wa Mwanzilishi wa maktaba hiyo, Jennifer Dickson, alisema  ameanzisha maktaba hiyo kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuhakikisha wakazi wa vijijini wanafikiwa huduma za maktaba waweze kupata maarifa.

"Maktaba hii inaitwa Martha Onesmo, ni kumuenzi bibi yangu, ni ndoto niliyoota tangu  nasoma kidato cha sita, ninafuraha kuwa ndoto hiyo imetimia. Pia ni Mchango wangu na wale walioniunga mkono, katika  juhudi za serikali zinazolenga kuboresha sekta ya elimu nchini", alisema.

Jennifer alisema maktaba hiyo imetokana na baadhi ya michango kutoka kwa wanajumuiya wa Msangeni, pia  itakuwa kituo cha mafunzo ya ujasiriamali.

Pia Jennifer aliwataka wananchi kujenga tabia ya kutumia huduma za maktaba kujisomea, wapate maarifa na kuachana na dhana potofu kuwa maktaba ni za wanafunzi, walimu na wasomi pekee.

Aidha, Jennifera alitoa shukrani kwa wafadhili  waliomwezesha kutimiza ndoto yake ya kuanzisha maktaba hiyo wakiwemo, Bayport Tanzania, Barick Gold Tanzania, Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT-MD).

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa  Bonaventure Rutinwa, alisema maktaba hiyo ni miundombinu ya kielimu inayomwezesha mtu au  watoto kupata elimu ya ziada kupitia usomaji wa vitabu.

Runtinwa alisema ni vyema watoto wakaanza kusoma na  kufahamishwa kuhusu umuhimu wa kutumia maktaba mapema katika hatua za utotoni.

"Tunasoma siyo kupata elimu ya shule pekee, bali kuboresha maisha yetu kwa ujumla na hii ni moja ya maana halisi ya kuwepo kwa maktaba kuwa;maktaba zimekusudiwa kwa ajili ya watu wote na si kwa ajili ya wanafunzi na walimu pekee",alisema.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa KKKT-MD, Askofu Chediel Sendoro, alimpongeza,  Jennifer kwa ubunifu wake ambao utachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Maktaba hii ijapokuwa ipo katika jengo la Kanisa, itatumika kwa watu wote bila kujali imani zao za kidini, lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata fursa ya kujiendeleza na kupata maarifa ya ziada kwa maendeleo yake binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema.

Aidha aliwapongeza wazazi wa mwanzilishi huyo na Dk. Linda Ezekiel, kwa malezi mazuri ya wazazi waliyompa binti yao ambayo yalimwezesha Jennifer, kuja na maono yenye lengo la kuchangia maendeleo ya Taifa
.