JESHI LA POLISI WAKAMATA WATUHUMIWA WATATU WIZI WA PIKIPIKI


 

Na MWANDISHI WETU

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata watuhumiwa mbalimbali wakiwemo wezi wa pikikipi na kukamata pikipiki zilizoibwa maeneo mbalimbali ya jiji na mikoa ya jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema operesheni ya kuwakamata wahalifu ilianza Februari 06, mwaka huu.

Amesema katika operesheni hiyo wamemkamata mtuhumiwa, mkazi wa Mlandizi, Omari Mlopa na wenzake wawili wakiwa na pikipiki 32, zilizoibwa na baadae kuzifanya zao kwa kuzikodisha kwa mikataba kwa watu mbalimbali na kujipatia pesa kila siku.

Muliro amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, umebaini watuhuhumiwa hao walibadilisha namba za usajili za pikipiki hizo na kuweka namba bandia zisitambulike.

Aidha Muliro amesema pikipiki 13 tayari zimetambuliwa na wamiliki wake.

Wakati huo huo Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, inaendelea na operesheni maalumu ya ukamataji wa watu wanaokiuka sheria kwa kutenda makosa ya usalama barabarani hasa kwa waendesha pikipiki (Bodaboda) na Bajaji.

Muliro amesema katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2023, makosa ya pikipiki yaliyokamatwa ni 179,174, walioandikiwa faini za papo kwa hapo ni 178,937, waliofikishwa mahakamani ni 237, waliohukumiwa adhabu ya kulipa faini 236, na mmoja alihukumiwa kifungo jela.

Amesema kwa kipindi cha Januari hadi Februari 2024 makosa ya pikipiki yaliyokamatwa 36,775, walioandikiwa faini za papo kwa hapo ni 36,754, waliofikishwa mahakamani ni 14, na mashauri 7 yapo kwenye ofisi ya Mashitaka ya Taifa.

Muliro amesema operesheni hiyo baadhi ya makosa yamekuwa yakijirudia kwa waendesha pikipiki na bajaji ni kutovaa kofia ngumu, kupita taa nyekundu, ulevi, kuzidisha abiria, kupita barabara za mabasi yaendayo haraka na kupakia abiria katika taa za kuongozea magari.

Amesema Polisi licha ya kuendelea kutoa elimu kuhusu uzuiaji wa makosa, ukamataji umelenga pia watu ambao wanakikaidi na kutotii sheria kwa kuendesha vyombo vya moto bila kujali na baadae kujikuta wakisababisha ajali.