CCM TANGA YAENDELEA KUCHAKAZA UPINZANI

Na MWANDISHI WETU, TANGA

UNAWEZA kusema Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga, kimeendelea kukichakaza Chama Cha Demokrasia na Maendeleo  (CHADEMA), hali iliyodhihirika katika mkutano wa Chama hicho cha upinzani kushindwa kufanya mkutano wake kwa kukosa wanachama.

Mkutano huo wa Chadema ulifanyika eneo la Kichangani, Wilaya ya Tanga  Mkoa wa Tanga, ambapo ilikusudiwa kuudhuriwa na viongozi wa Mkoa huo, lakini ulidoda baada ya watu kukosekana kabisa.

Chanzo hiki kilimtafuta, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, kutaka kufahamu hilo, alisema kushindwa kwa mkutano huo wa Chadema ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa Chama Cha Mapinduzi Tanga  kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.

"CCM Mkoa wa Tanga, tumejiimarisha vyema tuko imara, Chama  kiko hai kimeendelea kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya, elimu na miundombinu, hali ambayo imeendelea kuvutia wanachama wa vyama vingine kujiunga kutoka vyama vya upinzani ikiwemo Chadema," amesema.

Mwenyekiti Abdallah alimshukuru na kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, jambo ambalo limeendelea kuchochea Imani ya wanachama wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM.

Amesema kwa utekezaji wa miradi ya maendeleo unaoendelea Tanga, vyama vya upinzani vitaendelea kupukutika na kujiunga na CCM.