Programu ya maadili inavyochochea ufaulu shule za Alpha

Na MWANDISHI WETU

MKURUGENZI  wa Shule  za Alpha, Fatina Saidi amesema shule hizo zitaendelea kusimamia maadili kwa wanafunzi kukabiliana na changamoto za mmomonyoko wa maadili zilizopo katika jamii na kuchochea kiwango cha ufaulu.

Pia, shule hizo zimeendelea kutoa mafunzo ya urubani kupitia klabu ya Aviation ambayo inawaandaa wanafunzi wanaopenda masomo hayo, kwa masomo ya natharia na vitendo.

Ameyasema hayo  jana jijini Dar es Salaam katika kikao Cha watumishi wa shule hiyo na wazazi huku akisisitiza kuwa suala la maadili kwa wanafunzi wa shule hizo ni kipaumbele

"Katika shule zetu suala la maadili ni kipaumbele, atuangalii mtoto ni wa mzazi gani, tunatanguliza maadili na nidhamu yake, kwani ndio msingi mmoja wapo wa kumwezesha kufanya vizuri katika masomo yake," amesema

Alieleza kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kuwajengea msingi mzuri wanafunzi ambao watakuwa nao na kuwa wananchi wazuri wenye tija katika jamii.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Fatina amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawalea watoto wao katika msingi mizuri ya maadili tangu wakiwa utotoni kwani watakua nao kufikia mafanikio ya malengo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Maadili, Mwalimu Fulgence Kabilige, amesema katika kufanikisha hilo, wameeandaa mpango maalumu wa masomo ya maadili kwa wanafunzi wote unaojulikana kama Moral and Value Program ambapo unawafundisha masuala mbalimbali ikiwemo heshima na nidhamu kwa wazazi, mahusiano sahihi.

"Chanzo cha kuanzisha mpango huo wa masomo ya maadili ni kuwajenga wanafunzi kuwa na nidhamu, ambayo ni msingi wa kufanya vizuri katika masomo yao na kufikia ndoto zao.

" Pia, lengo la masomo hayo ni kuwajenga kimaadili wanafunzi wasiharibiwe na mabadiliko ya mmomonyoko wa maadili yanayo athiri mataifa mengi, " amesema.

Ameeleza kuwa, masomo hayo yatawasaidia katika kuwajenga katika uwajibikaji mzuri wa sasa katika masomo na baada ya masomo watakapo ajiriwa na watakapo kuingia katika ndoa zao.

Aliwataka wazazi kuendelea kuzingatia maadili kwa watoto wao huku akiahidi kuwa shule za Alpha zitaendelea kuwalea katika maadili wafikie malengo yao ya kimasomo.

Ametaja klabu zingine zinazofundishwa shuleni hapo ni ujasiriamali, maigizo, kuomba, muziki, urembo, kompyuta, uchoraji,  urubani  ambapo watoto wao hupelekwa nchini kenya katika mafunzo ya vitendo.