WAKUFUNZI WALIOSHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022 WILAYANI MKALAMA WATUNUKIWA VYETI

Na HEMEDI MUNGA 

WATAALAMU mbalimbali wilayani Mkalama, mkoani Singida walioshiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya  mwaka 2022 wamefurahishwa na zawadi ya vyeti kutoka kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa.

Aidha, Dk. Chuwa ametoa vyeti hivyo ambavyo vinathibitisha kuthamini na kutambua utendaji wao bora uliofanikisha zoezi hilo muhimu kwa Taifa.

Akizungumza baada ya kugawa vyeti hivyo kwa washiriki 726 wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Asia Messos amemshukuru na kumpongeza Dk. Chuwa kwa kutoa vyeti ambavyo vimetambua mchango wa walioshiriki na kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huo.

Asia amegawa vyeti toka kwa kiongozi huyo kwa  wakufunzi wa wilaya hiyo ambao waliotoa mafunzo ya ukarani, usimamizi wa maudhui na TEHAMA wakati wa zoezi hilo.

"Nimekabidhi vyeti kwa baadhi ya Wakufunzi wa Wilaya na Makarani walioshiriki katika zoezi la Sensa la mwaka 2022 ndani ya Halmashauri yetu," amethibitisha.

Aidha, amewapongeza wataalam hao  kwa sababu walishiriki  zoezi hilo kwa umakini na uzalendo mkubwa.

Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchakata, kuchambua, kutathmini, kuchapisha, kusambaza na kutunza takwimu za kidemografia, kiuchumi na mazingira wanayoishi katika nchi kwa kipindi maalum. 

Aidha, Utaratibu huu huwezesha kupatikana kwa taarifa za msingi za kitakwimu kama idadi ya watu wote kwenye nchi kwa umri, jinsi, hali ya ulemavu, hali ya elimu, shughuli za kiuchumi, hali ya makazi, vizazi, vifo na nyingine kama zilivyoainishwa katika dodoso la Sensa.