Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba ameendelea kuwaeleza wananchi nchini namna ambavyo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan hata asipokanyaga katika maeneo yao bado amekwisha wapelekea ujumbe wa namna ambavyo ameendelea kuwaheshimu na kuwajali kivitendo na kuwa yupo pamoja nao.
Dk. Nchemba ametoa elimu hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi mjini Kiomboi, wilayani Iramba mkoani Singida.
"Ndugu zangu tunakila sababu ya kuiunga mkono serikali, hakika imefanya mambo makubwa," amesema.
Akizungumza kuhusu nishati ya umeme, Dk. Nchemba ameeleza kuwa serikali imefanya kazi kubwa nchini huku kwa wilaya hiyo vijiji vyote 70 vimekwishafikiwa na umeme.
Amesema kuwa hivi sasa kuna takribani sh bilioni 700 zinakwenda kujaziliza umeme kwenye vitongoji na katika maeneo ya mjini ambayo bado kuna watu wanajenga nyumba mpya, hivyo suala la umeme ni endelevu.
Mbali na hayo, Dk. Nchemba amebainisha kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere kukamilika, hivyo ipo tofauti kubwa hivi sasa ukilinganisha na wakati wa nyuma kuhusu kukatika katika kwa umeme.
Amedokeza kuwa hivi karibuni wataachia kipande kingine ambapo umeme utaendelea kusambazwa katika vitongoji na kufanikiwa kuendelea kufungua uchumi wa wananchi.
Aidha, amesema Rais Dk. Samia alipeleka skimu za umwagiliaji katika maeneo tofauti nchini ikiwemo katika wilaya hiyo kwa lengo la kuwaongezea watu kipato cha mtu mmoja mmoja.
"Hili linawatengenezea wananchi kipato cha mtu mmoja mmoja na kuwaondoa kwenye umasikini, hakika hizi ndio kazi ambazo serikali inazifanya chini ya Jemedari wetu Rais Dk. Samia," amesisitiza Dk. Nchemba.
Ameeleza kuwa haya anayoyafanya Rais Samia ndio njia sahihi na halisi ya kuwaondolea watanzania umasikini.
Amesema kuwa, leo hii hadi vijijini wanapata miradi ya umwagiliaji ya zaidi ya sh bilioni 30, hivyo wataweza kuvuna mazao yao mara mbili.
Aidha, ameongeza kuwa katika sekta ambazo zinatoa ajira kwa watu wengi zitapata mavuno zaidi, hivyo wataweza kubadilisha maisha yao.
Pia, amesema Rais Dk Samia ameendelea na ujenzi wa barabara za vijijini ni dhahiri wakulima watapeleka mazao yao sokoni na kuweza kuongeza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja, hatimae kupunguza umasikini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Suleiman Mwenda ameendelea kumuomba Waziri huyo, kuwafikishia salam kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa wanampongeza, wanamshukuru na kumuombea afya njema muda wote.
Aidha, amemuhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono muda wote huku wakiahidi kumpa kura tele ifikapo 2025.