WATAALAMU WA TAALUMA YA UTUNZAJI KUMBUKUMBU NA NYARAKA KUPATIWA MAFUNZO

Mwenyekiti wa Chama cha Menejiment ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRMPA), Devotha Mrope.

Na MWANDISHI WETU

Mwenyekiti wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), Devotha Mrope, amezindua mafunzo maalumu yanayolenga kujenga uwezo wa kitaaluma kwa wataalamu wa taaluma ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini.

Devotha ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari, Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watumishi wa umma na taasisi binafsi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na uadirifu katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.

"Mafunzo haya yatawakilisha juhudi za TRAMPA katika kujenga uwezo na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini Tanzania. Tunajitahidi kuhakikisha kuwa wataalamu wetu wanapata mafunzo na maarifa yanayohitajika ili kuhakikisha kuwa taarifa na nyaraka zinatunzwa kwa weledi na uadilifu", amesema.

Devotha amesema mafunzo hayo yamepangwa kufanyika Mei 6 hadi 9, 2024 mkoani Iringa katika ukumbi wa Masiti Grand Hall na yanatarajiwa kuhudhuriwa na wataalamu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Amesema hiyo ni fursa kwa washiriki kujifunza mbinu mpya na  bora za utunzaji wa kumbukumbu, uadilifu katika utunzaji wa siri za ofisi na njia za kisasa za usimamizi wa nyaraka za taasisi.

Pia Devoth amesema kwa kuzingatia thamani ya mafunzo hayo, washiriki watalazimika kulipia gharama ya ushiriki shilingi 400,000, ambayo itagharamia uendeshaji wa mafunzo kwa muda wa siku nne. 

 Devotha ametoa wito kwa waajiri kuwawezesha watumishi wao kuhudhuria mafunzo hayo na kuwalipia stahiki zao. 

Aidha Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wanataaluma uthibitisha ushiriki wao mapema ili kurahisisha maandalizi ya mafunzo hayo muhimu ambayo yatawezesha kuboresha utendaji na ufanisi katika utunzaji wa taarifa za umma na za binafsi.

“kada hii ni miongoni mwa kada zinazoongozwa na mifumo mingi, sambamba na miongozo kulingana na wakati. Hivyo, inalazimu wataalamu wajengewe uwezo kuendana na mazingira ya wakati husika” amesisitiza Bi. Devotha.