TIMU YA WATUMISHI MANISPAA YA SINGIDA YAISHUSHIA KIPIGO KIZITO WATUMISHI WILAYA YA IRAMBA MKOANI SINGIDA
![]() |
| Timu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida. |
Na HEMEDI MUNGA, Iramba
TIMU ya mpira wa miguu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida imekubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Timu ya Watumishi Manispaa ya Singida .
Mchezo huo, umechezwa katika uwanja wa Mabatini wilayani Iramba mkoani hapa.
Akizungumza na Mwandishi wetu, baada ya mchezo huo kuisha Kapteni wa Timu ya Manispaa, Jafari Ashrafu amesema walifanya maandalizi kwa sababu walifahamu wanakuja ugenini hivyo, ni lazima wapate ushindi utakaowahamasisha wapinzani warejeane hivi karibuni.
Aidha, ameeleza kilichowasukuma kuwa na mchezo huo wa kirafiki ni kuendeleza udugu kwa sababu wote wapo mkoa mmoja na kudumisha afya zao.
Pia, ametoa wito kwa watumishi wakiwemo vijana mbalimbali waendelee kuamka kufanya mazoezi kwa sababu mazoezi ni sehemu ya afya.
"Ili uweze kuwa mtumishi bora ni lazima ufanye mazoezi kwa lengo la kuifanya afya iendelee kuwa bora," amesema.
Kwa upande wa Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani hapa, Constantine Kihwele amesema wameyapokea matokoe ya mchezo huo na wanajipanga kwa sababu wiki ijayo watakua na mchezo mwingine dhidi ya Timu ya Waandishi wa Habari wa mkoa huo.
"Tunashukuru mchezo ulikua mzuri, hivyo tumefanya mazoezi ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa," amesema na kuongeza kuwa :
"Michezo inasaidia kuimarisha afya zetu hasa ukizingatia watumishi tunatumia muda mwingi tukiwa ofisini, hivyo tunapopata michezo inaendelea kutujenga."
Michezo hiyo ya kirafiki inaendelea ikiwa nisehemu ya kuendelea kutekeleza agizo la Majaliwa alilolitoa Mei 11, 2024 wakati akiwa jijini Mbeya.
Aidha, Majaliwa aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuharakisha kutenga maeneo kwa lengo la wananchi kufanya mazoezi yatakayowakinga na magonjwa yasioambukiza.
![]() |
| Timu ya Watumishi Manispaa ya Singida. |
Reviewed by Gude Media
on
June 01, 2024
Rating:

