KMC FC YAREJEA NYUMBANI KUWAVAA NAMUNGO


 Kikosi cha Timu ya KMC FC kesho kitashuka katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam kikiwakaribisha Namungo ya Ruangwa Mkoani Lindi katika mchezo utakaopigwa saa 16 00 jioni.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana itakuwa nyumbani kwenye mchezo huo ikiwa ni mara baada ya kupita takribani mwezi mmoja KMC FC kucheza kwenye uwanja huo na kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Polisi Tanzania uliochezwa Disemba 22 mwaka jana.

Kikosi hicho cha wana Kino Boys kimeshajiandaa kikamilifu kuwakabili Namungo licha ya kuwa ni mchezo wenye ushindani na kwamba kama Manispaa ya Kinondoni imejipanga kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

"Tunakwenda kwenye mchezo mgumu lakini tunakila sababu ya kuhakikisha kwamba Timu inapata matokeo mazuri kutokana na ushindani uliopo kwasasa huku ukizingatia Msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2022/ 2023 unakwenda ukingoni.

"Tunapokwenda kwenye mchezo wa kesho pamoja na kwamba tupo nyumbani lakini tutaingia tukiwaheshimu wapinzani wetu kutokana na kwamba wanakikosi kizuri na benchi lao la ufundi pia ni zuri, lakini KMC FC inawachezaji bora zaidi ambao siku zote wamekuwa wakiipa thamani kwakuipambania Manispaa ya Kinondoni ili kupata matokeo chanya.

Kwa upande wa Afya za wachezaji, wote wako vizuri wana hari na morali huku tukiwa na ufahamu kuwa mashabiki zetu wamekuwa na shauku ya kuona burudani kwenye uwanja wa Uhuru na hivyo tumejiandaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kwenye mchezo huo wanaondoka na furaha.

KMC FC itawakosa wachezaji wawili muhimu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ambao ni Awesu Ally Awesu pamoja na Hance Masoud Msonga huku wachezaji wengine wakiwa tayari kwa mtanange huo.

KMC FC inawaomba mashabiki zake kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho ili kuishuhudia Timu yao ikipambana kuwapa burudani  na hivyo kusonga mbele kwa kuvuna alama tatu muhimu na kuendelea kujiweka vizuri katika msimamo wa Ligi ambapo ipo kwenye nafasi 10 huku ikiwa imecheza jumla ya michezo 20 na kukusanya alama 23.


Imetolewa na

Ofisa Habari na Mawasiliano KMC FC.