KUELEKEA PAMBANO LA WATANI WA JADI SIMBA NA YANGA, JESHI LA POLISI LIMETOA ONYO KWA MASHABIKI WENYE TABIA YA KUWASHAMBULIA WAAMUZI


 

Na Mwandishi Wetu

Kuelekea mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetoa onyo kwa baadhi ya mashabiki wenye tabia ya kuwashambulia waamuzi wasaidizi.

Pia Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeshauri mashabiki kutokwenda uwanjani na matokeo mfukoni.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo, mechi hiyo inatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Amesema vitendo hivyo huwa vinafanywa na baadhi ya mashabiki wasiokubaliana na maamuzi kwa chupa za maji au chupa zenye vimiminika vinavyodhaniwa kuwa na haja ndogo.

Pia Murilo amesema polisi hawatavumilia mashabiki wenye tabia ya kuharibu miundombinu ya uwanja wa Benjamin Mkapa,  kama kuharibu mabomba ya vyoo na bafu, viti vya uwanja huo.

Amesema watakaofanya vitendo hivyo watakamatwa wakati huo huo au baada ya mchezo, kutegemea mazingira mtuhumiwa atakapokamatwa.

Murilo amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na mchezo katika uwanja huo

"Tunawatoa hofu mashabiki watakaofika kushuhudia mchezo huo kuwa usalama  utakuwa umeimarishwa kwa kiwango cha juu maeneo yote ya kuzunguuka uwanja huo ndani, nje na barabarani", alisema.

Pia Murilo amepiga marufuku kwa mtu yoyote kwenda na silaha uwanjani ispokuwa vyombo vya dola vyenye dhamana jukumu la usalama wa eneo hilo.