WANNE WA FAMILIA MOJA WAMEFARIKI BAADA YA KUVUTA HEWA CHAFU YA MOSHI WAKIWA WAMELALA



Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro

Na Mwandishi Wetu

Watu wanne wa familia moja wamepoteza maisha baada ya kuvuta hewa chafu ya moshi kutoka kwenye jenereta walilowasha ndani ya nyumba na baadaye kulala.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne, amesema tukio hilo lilitokea Aprili 19, Chang’ombe, wilayani Temeke, Dar es salaam.

Muliro amesema taarifa zilieleza kuwa Aprili 18, 2023 saa 4.00 usiku watu hao waliwasha jenereta baada ya umeme kuzimika na kuliweka ndani ya nyumba.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha watu hao walipoteza maisha baada ya kuvuta hewa inayodaiwa kuwa ni hewa chafu ya moshi iliyokuwa inatoka katika jenereta baada ya kuwashwa.

Muliro amewataja waliopoteza maisha ni Kazija Mohamed (21), Munir Ibrahim (7), Munira Ibrahim (6) Muyyat Ibrahim (3). 

Pia Muliro amesema mume na mke ambao ni Ibrahim Juma (28) na Aisha Ayubu (29) wote wakazi waKilimahewa, Chang’ombe hali zao sio nzuri na wanaenedelea kupatiwa matibabu katika Hospitaliya Taifa ya Muhimbili.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na mamlaka zingine.