MWENGE WA UHURU KUPITIA MIRADI YA BILIONI 23 DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

MWENGE wa Uhuru umeanza mbio zake mkoani Dar es Salaam, ambapo utatembelea miradi 32 yenye thamani ya sh. bili.23.4.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albart Chalamila, wakati akiupokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge.

Chalamila alisema,  miradi hiyo iko katika hatua mbalimali, ambapo baadhi imekamilika.

"Vilevile Mwenge wa Uhuru utakapokuwa inapita, utakuwa ukihamasisha, shughuli za maendeleo,upendo na amani na uzalendo," alisema Chalamila.

Alieleza utakimbizwa katika Wilaya za Temeke, Kigamboni, Ilala,Ubungo kisha Kinondoni, ambapo Mei 29 utaondoka kwenda Mjini Magharibi, Zanzibar 

Awali akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kunenge alisema, katika Mkoa wa Pwani ilipitia miradi 99 yenye thamani ya sh. trilioni 4.46 ambapo hakuna miradi uliokataliwa 

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamis Munkunda, alisema, Mwenge wa Uhuru utapitia miradi sita yenye thamani ya sh.13.6.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa,  Abdallah Shaib Kaim,  amesisitiza wananchi kuzingatia ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 unaosisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira,kutunza vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa taifa.

Pia Kaim aliitaka jamii  kupinga vita rushwa, kuhimiza lishe bora, kupambana na maralia na maambukizi ya ukimwi.