RAIS SAMIA ASHIRIKI MKUTANO WA DHARURA SADC NCHINI NAMIBIA

RAIS Samia Suluhu Hassan, amehudhuria Mkutano wa kujadili hali ya Usalama Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), nchini Namibia.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, amesema mkutano huo wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force Intervetion (FIB) umefanyika mjini Windhoek, Namibia.

Zuhura amesema mkutano umetoa tena wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikiria nchini humo.

Amesema pia mkutano umewasihi wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Zuhura amesema mkutano umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo ili kuleta amani endelevu, usalama na ustawi kwa wananchi wa Kongo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla.

Pia Zuhura amesema kwa upande mwingine mkutano umeidhinisha kupeleka Kikosi cha SADC kutoka katika kikosi cha kudumu cha jumuiya hiyo ili kuunga mkono DRC iweze kurejesha amani na usalama.

Aidha mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Rais wa Namibia, Dkt. Hage Geingo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Balozi Tete Antonio, Waziri wa Ulinzi Jamhuri ya Malawi, Harry Mkandawire na Balozi wa Zambia nchini Namibia, Stephen Katuka.