WAKANDARASI WAZAWA WATAKIWA KUWA MABALOZI WAZURI KWA KUTEKELEZA MIRADI YENYE VIWANGO NA KUIMALIZA KWA WAKATI

 Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya, amewataka wakandarasi wazawa  kuwa mabalozi wazuri kwa kufanya kazi nzuri kwa kuzingatia viwango na kukamilisha miradi kwa wakati.

Kasekenya alisema hayo, wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Bodi ya Wasajili wa Makandarasi, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, na kwamba wazingatie muda wa kumaliza kazi zao.

Alisema kukamilika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo  kutaisadia Serikali ipate thamani ya fedha katika miradi yote itakayotekelezwa kwa viwango na kukamilika kwa wakati.

"Wakandarasi wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi yetu na inapotokea Wakandarasi wanashindwa kutimiza wajibu wao wanachelewesha wananchi kupata huduma zilizokusudiwa na pia kuisababishia hasara Serikali", alisema.

Naye Meneja wa Kitengo cha utoaji fedha za Biashara wa Bank of Africa Tanzania, Jessica Mizambwa, alisema benki hiyo imewarahisishia Wakandarasi upatikanaji wa mikopo na dhamana za benki, ambazo zitawarahisishia vigezo vya kupata mikataba mbalimbali ya kufanikisha miradi yao.

Jessica amesema benki hiyo inatoa huduma maalumu ambazo ni suluhisho  katika kufadhili miradi mbalimbali ya wakandarasi, zikiwemo dhamana ya Zabuni inayotoa dhamana ya hadi Sh. Bilioni 1 ndani ya saa 24, Dhamana ya Malipo ya Mapema, Dhamana ya Utendaji kazi, punguzo la ankara, mikopo.

Amesema huduma za kifedha kusaidia biashara zinalenga kukuza ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa kuvuka mipaka na hata ndani.

"Kupitia mpango wa Benki of Afrika Tanzania, wa kuwezesha wakandarasi, hasa wadogo, wanaweza kupata mashine bora za kufanyia kazi na kuweza kufanikisha kutekeleza miradi yao, benki itawawezesha wakandarasi kupata mashine na kuondoa tatizo la wakandarasi kushindwa kutoa huduma kwa kukosa mashine au fedha", alisema.

Pia Jessica amesema BOA Tanzania, inawezesha wafanyabiashara za aina mbalimbali ikiwemo wakandarasi, waagizaji bidhaa kutoka nje, na wauzaji bidhaa nje ili kuweza kupunguza uwezekano wa kupata hasara zinazohusiana na kufanya biashara  za nje ya nchi.


NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi. Godfrey Kasekenya (katikati), akikabidhi kwa Meneja wa Kitengo cha utoaji fedha za Biashara wa Bank of Africa Tanzania, Jessica Mizambwa, tuzo ya  kushiriki katika mkutano wa Mwaka wa Bodi ya usajili wa wakandarasi,  jijini Dar es Salaam,  mwishoni mwa wiki.
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya (katikati), akipata maelezo  kutoka kwa Meneja wa Kitengo cha utoaji fedha za Biashara wa Bank of Africa Tanzania, Jesca Mizamba, kuhusu  huduma mbalimbali zinazotolewa na  benki hiyo, wakati akikagua  banda la maonyesho la benki hiyo katika Mkutano wa mwaka wa Bodi ya usajili wa wakandarasi,  jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.