BANK OF AFRICA-BAJETI YA SERIKALI INA MWELEKEO WA KUKUZA UCHUMI


Bank of Africa Tanzania (BOA),  imeipongeza baejeti ya Serikali kuwa ina mwelekeo wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuwezesha wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Adam Mihayo, alisema hayo jana  wakati akitoa maoni kuhusu  bajeti ya Serikali ya kipindi cha mwaka 2023/2024 iliyosomwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Alisema bajeti imekuwa na mwelekeo wa utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara, ambapo baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na serikali kupunguza urasimu na majukumu kinzani katika taasisi za umma na kupunguza baadhi ya kodi na tozo zisizo na tija.

Mihayo alisema bajeti  imekuwa na mwelekeo wa Serikali kuendelea kutekeleza Sera za Bajeti na Fedha zinazolenga kuwezesha sekta binafsi ambapo hatua hizo ni pamoja na kulinda thamani ya shilingi na kuhakikisha akiba ya fedha za kigeni ni toshelevu.

Amesema Bank  of Africa Tanzania imejipanga kupitia kuwekeza katika ubunifu wa huduma , bidhaa zitakazosaidia kuboresha Maisha ya watanzania waliowengi pamoja na kukuza uchumi wa taifa. 

Amesema benki imelenga kuhakikisha kasi ya mabadiliko kila wakati inaendana na mabadiliko ya mahitaji ya wateja na watanzania kwa ujumla.

Pia Mihayo amesema  inaendelea kutoa huduma bora mbalimbali nchini na inatilia mkazo katika kuwezesha kundi la wafanya biashara  wadogo na  wa kati (SME) inayounaoenda na ajenda ya Serikali ya awamu ya sita ya kukuza ushirikishwaji wa huduma za kifedha nchini Tanzania.

Amesema BOA inaendelea kuboresha huduma zake za kidijitali zinazotolewa na benki zinaendelea kuboreshwa zaidi huduma zake za kidigitali,  kuvutia wateja zaidi na kuwapa urahisi wateja wa Benki katika upatikanaji wa huduma zake.