STANDARD CHARTERD BANK WAENDELEZA MPANGO WA KUDHIBITI TAKA ZA PLASTIKI BAHARINI

 Benki ya Standard Chartered, imeendelea kutekeleza mpango wake wa  kupunguza kiasi cha taka za plastiki zilizotupwa baharini na kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Herman Kasekende, akizungumza wakati wa walipofanya usafi katika ufukwe wa Kibo, Mbezi, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, ikiwa ni  Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Dunia, amesema juhudi zinazofanywa na benki hiyo ni kuimarisha utunzaji wa mazingira.

Kasekende amesema benki hiyo inatambua umuhimu wa Siku ya Mazingira Duniani na imedhamiria kuendeleza utamaduni wa utunzaji wa mazingira ndani ya benki na jamii kwa ujumla.

"Mpango wa kusafisha ufukwe unaonyesha dhamira yetu ya dhati ya kutunza mazingira, siku zote tumekuwa tukiongozwa na adhama yetu ya kuwa na mifumo ya kibishara yenye uendelevu na
tunatambua kwamba mafanikio yetu yanahusiana sana na ustawi wa jamii ambazo tunafanya kazi”, amesema Kasekende

Amesema kama  taasisi ya kifedha, wana fursa ya pekee ya kuleta athari chanya kwa kuwekeza katika suluhisho endelevu na kusaidia jitihada zinazokabiliana na changamoto za mazingira.

Pia Kasekende amesema Benki ya Standard Chartered itahakikisha inajumisha mbinu endelevu katika uendeshaji wake na kuwahimiza wafanyakazi wake kuwa mawakala wa mabadiliko,  kwa kujihusisha na shughuli zenye tija ikiwemo  kusafisha ufukuwe wa bahari.

Amesema benki inalenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira, ambapo
imetekeleza mipango kadhaa ya mazingira, ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika kufanya mapinduzi ya kibenki kwa kuleta huduma za kidijitali, kupunguza kiwango cha kaboni na kusababisha asilimia 90 ya miamala kufanywa kidijitali na kuondoa foleni katika matawi.

Kasekende amesema benki imeboresha udhibiti wa taka, ikisababisha ongezeko la asilimia 360 katika taka zinazoweza kuchakatwa na kupungua kwa asilimia 40 katika jumla ya taka zinazozalishwa kila mwaka na imepanda miti zaidi 3,000.