DUWASA YAANIKA MKAKATI KUPELEKA MAJI KIBAIGWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph, ameeleza mkakati wa kupeleka maji katika mji wa Kibaigwa kwa kuchimba visima kukabiliana upungufu wa maji.

Mhandisi Aron alitoa maelezo hayo baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, kumtaka kujibu mbele ya wananchi namna ya kuondokana na kero ya upungufu wa maji.

Alisema DUWASA ambayo imekabidhwa kuhudumia mji huo Juni 9 mwaka huu inatoa maji kwa mgao kutokana na uzalishaji kuwa mdogo ikilinganishwa na mahitaji.

Alisema mahitaji ya maji ni lita milioni 3.7 kwa siku na uwezo wa kuzalisha ni lita milioni 2.3 na hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 1.4 kwa siku.

“Hata hizo lita miloni 2.3 hatuzizalishi inavyotakiwa kutokana na changamoto ya umeme na tumekuwa tukizalisha kwa saa 10 hadi saa 12, hivyo wananchi hawa wanaweza kupata maji mara mbili ya wanavyopata sasa kama tutakuwa na umeme wa uhakika.”

Mhandisi Aron alisema baada ya kukabidhiwa kutoa huduma, DUWASA imetembelea chanzo cha maji na kubaini kumilikiwa na wananchi hivyo kuhitaji ulipaji fidia ili wananchi waachie bonde hilo.

Mhandisi Aron alimuomba Katibu Mkuu amsaidie kwa wananchi waridhie kutoa maeneo yao ili DUWASA ianze kuchimba visima vya maji hata kabla ya ulipaji wa fidia kwani mahitaji ya maji ni makubwa.

 “DUWASA ndio imeingia, wananchi wa Kibaigwa watupime baada ya miezi sita, pamoja na kuwa ni maeneo yenu niruhusuni nianze kuchimba kisima hata kabla ya kuwalipa fidia, niwahakikishie huduma ya maji itaimarika.” anasema Mhandisi Aron.

Kuhusu hoja ya wananchi ya kufungwa kwa vichoteo vya maji, Mhandisi Aron alisema DUWASA haitafunga hata kimoja na kuwataka wanaosimamia kuhakikisha wanalipa ankara za maji kwa wakati.“

Vichoteo vya maji vinavyofanya vizuri havita fungwa hata kimoja, lakini changamoto iliyopo wanaoviendesha hawalipi Ankara zao kwa wakati na mpaka sasa vinamadeni zaidi ya shilingi milioni 6,” anasema Mhandisi Aron.

Kuhusu hoja ya gharama ya maunganisho ya maji, Mhandisi alisema serikali inalifanyia kazi na inatarajia kuja na bei elekezi.