ILALA YASAINI UJENZI WA BARABARA ZA SH. BILIONI 5.8

Na MWANDISHI WETU

HALMASHSURI ya Jiji la  Dar es Salaam, imetiliana saini na kampuni tatu za ujenzi kujenga barabara zenye thamani ya sh. bilioni 5.6.

Akizungumza   wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba hiyo, jana, Meya wa jiji hilo,  Omaray Kumbilamoto, amesema, ujenzi huo utahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, zege na makaravati.

Alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa usimamizi imara wa maendeleo kwani kujengwa kwa miundombinu hiyo kutasaidia kuwaondolea wananchi changamoto ya usafiri.

"Fedha za utekelezaji wa miradi hii zipo. Wito wangu kwa wakandarasi tumekubaliana kazi hii iwe imekamilika katika kipindi cha miezi sita. Ikamilike kwa wakati na inaweza kukamilika hata kabla ya muda huo. Mjiongeze", amesema Meya kumbilamoto.

Aliwataka makandarasi kufanya kazi usiku na mchana kama ilivyo kwa miradi mingine inayotekelezwa na serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo,  aliyeshuhudia utiaji huo wa saini, amempongeza Rais DK. Samia, kwani ndiyo chachu ya  cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kutenga kiasi cha sh. bilioni 6.2 kwaajili ya miradi wa ujenzi wa barabara.

Alisema kiasi hicho cha Sh. bilioni 5.8 za mikataba iliyosainiwa jana kinatoka katika kiasi cha sh. bilioni 6.2 zinazo tokana na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo .

" Ujenzi wa barabara hizi ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM, hivyo tunaahidi kuisimamia kikamilifu", amesema Mpogolo.

Mwenyekiti wa CCM  wa Wilaya ya Ilala Said Side, amewataka wakandarasi kufanya kazi kwa weledi, ubora na kuzingatia thamani ya fedha.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru, amesema, ujenzi huo utanufaisha majimbo yote matatu ya jiji hilo ambayo ni Ilala, Ukonga na Segerea.

Alisema ujenzi utasimamiwa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA).

Mhandisi Mafuru, alitaja kampuni  zilizopewa zabuni hiyo ya ujenzi  ni Southern Link, iliyoingia mkataba wa sh. bilioni 1.9, itakayo jenga barabara katika Jimbo la Ukonga zenye urefu wa kilomita 1.4.

Barabara hizo ni Pugu-Majohe,Kitunda-Kivule na Mwanagati.

Kampuni nyingine ni M.J.S iliyosaini mkataba wa sh. bilioni 1. 9, wa ujenzi wa barabara za Nyati, Rufiji na Mchikichi ni kwa kiwango cha lami katika Jimbo la Ilala.

Pia itajenga barabara za Mtende ni na Sauthern kwa kiwango cha zege.

Mafuru ameitaja kampuni nyingine kubwa niabibo construction Limited, iliyoingia mkataba wa ujenzi wa caravati kubwa la boksi, katika eneo la Kufufua Majoka, Jimbo la Segerea, kwa thamani ya sh. milioni 650.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabibo, Cloud Chalrz, amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kazi hiyo inakamilika katika kipindi cha miezi sita.

Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam. Mhandisi, Amani Mafuru
(kushoto), akibadilishana mkataba na Mkandarasi wa Kampuni ya Southern
Link Limited, Johnbosco Mosha, baada ya kutia saini mkataba wa ujenzi wa
barabara zenye urefu kilomita 1.4,  wilayani Ilala.