UJENZI GHOROFA SITA HOSPITALI MBAGALA KUGHARIMU SH. BILIONI 10.4

Na MWANDISHI WETU 

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamisi Munkunda, amemtaka Mkandarasi Kampuni ya Group Six International, iliyopewa kandarasi ya upanuzi wa Hospitali ya Mbagala Rangitatu kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Ametoa agizo hilo Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini  mkataba  wa  ujenzi wa jengo la ghorofa sita ambapo mpaka kukamilika kwake unatarajia kugharimu kiasi cha sh. bilioni 10.4.

Mkuu wa Wilaya amesema, Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha kiasi cha sh. bilioni 2 za kuanza kwa ujenzi huo, hivyo hatarajii kuona kazi hiyo ikichelewa kuanza kwa mradi huo.

"Mradi huu kwetu ni ahsante kwa Rais, tunaomba umpe heshima yake ikiwezekana mradi huu ukamilike kabla ya miezi hiyo 24", amesema  Munkunda.

Awali Meya wa Manispaa ya Temeke,  Abdallah Mtinika, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulipa kodi na tozo mbalimbali zitakazoiwezesha halmashauri hiyo kupata fedha za kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya,  alimhakikishia mkuu  Wilaya kuwa ataendelea kusimamia fedha za Serikali kikamilifu ili ujenzi huo uendane na thamani halisi ya fedha.

Ujenzi huo wa ghorofa sita utakapokamilika utasaidia kuondoa msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo na kusaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Wilaya ya Temeke na wilaya za jirani.