WANAWAKE WAJASIRIAMALI WA BATIKI DAR WAMUOMBA RAIS SAMIA FURSA ZA MASOKO YA KIMATAIFA

Na Mwandishi.Wetu

Wanawake wanaojihusha na utengenezaji mavazi ya batiki Mkoa wa Dar es Salaam, wamemuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwasadia kuwaunganisha na fursa katika masoko ya kimataifa .

Wameyasema hayo, wakati mafunzo  kuhusu, mitaji na akiba kupitia benki, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake Watengeneza Batiki Soko la Mchikichini wilayani Ilala (KIKUWASO), Elinaike Kimati,alisema changamoto kubwa  inayowakabili ni soko la kueleweka la bidhaa za batiki hususan masoko ya kimataifa nje ya nchi.

"Hivi sasa kuna soko la kimataifa la Afrika Mashariki, sisi wanawake watengeneza batiki hatuna mtu wa kutushika  mkono. Tunamwomba  Rais DK. Samia, atusaidie,"alieleza Elinaike.

Alibainisha mbali na kutengeneza bidhaa bora za kimataifa za mavazi ya batiki  lakini bado  bidhaa hizo hazifikiwi kikamilifu na wateja hivyo kuwafanya wanawake hao kushindwa kupata  kipato cha kuridhisha.

Sambamba na hilo, walimwomba Rais DK. Samia, kuwakumbuka katika mikopo ya asilimia 10 ya pato la ndani inayotolewa na halmashauri.

Alisema, vikundi hivyo vimekuwa vikikosa mikopo kutokana na wanachama wake kutoka katika maeneo tofauti.

" Tangu mikopo hiyo ianze kutolewa sisi wanawake watengeneza batiki hatujanufaika nayo kwa sababu halmashauri wanasema tunatoka katika maeneo tofauti. 

Sisi ndiyo vikundi vya ujasiriamali wanawake tunakosa mitaji," alieleza 

Katibu wa KIKUWASO, Adela Swai, alisema asilimia kubwa ya batiki zinazovaliwa katika nchi nyingi chimbuko lake niSoko la Mchikichini nchiniTanzania.

"Watu wengi wanahitaji bidhaa hizi kimataifa lakini tumekosa mtu wa kutufikisha katika masoko makubwa ya kimataifa. Serikali yetu ni sikuvu itusaidie" alisema  Adela.

Pia aliomba wauzaji wa malighafi za batiki kupunguza gharama hali itakayo waongezewe ufanisi kwani hivi sasa gharama ni kubwa.

Kwa upande wa Eunice Tugala, ambaye ni mtengenezaji wa batiki kutoka Msasani Wilaya ya Kinondoni, aliomba serikali pindi inapopatikana fursa ya maonyesho ya kimataifa basi wakumbukwe kushirikishwa.

"Serikali itaangalia hata kutudhamini kwa  nusu ya gharama. Tuko tayari kushiriki popote na bidhaa bora tunazo," alisema Eunice.

Akitoa elimu ya akiba na mikopo, Ofisa Uhusiano wa Benki ya Azania Abishua Mganga, alisema kwa kutambua changamoto ya mitaji na akiba, benki hiyo imeanzisha akaunti maalumu ya Mwanamke Hodari.

Alieleza akaunti hiyo  inafunguliwa bure, haina makato wala riba hivyo kuwashauri kuchangamkia.

Mganga alibainisha mjasiriamali mali anapokuwa na akaunti hiyo anauwezo wa kukopa hadi mara nne ya akiba iliyopo katika akaunti yake na anaweza kukopa hadi sh. milioni 500 kwa masharti nafuu na atatakiwa kurejesha asilimia moja tu kwa mwezi ya mkopo.

Katibu wa Kikundi cha Wanawake Watengeneza Batiki Soko la Mchikichini (KIKUWASO) Adela Swai akizungumza  wakati wa mafunzo ya akiba na mitaji yalitoandaliwa na kikundi hicho kwa kushirikiana na Benki ys Azania, Dar es Salaam.