DKT. SHEKALAGHE: WANANCHI WANATEGEMEA HUDUMA BORA WANAPOFIKA HOSPITALINI

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe leo amekutana na Wakurugenzi Watendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili-MOI ili kujadiliana namna ya kuendelea kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa na hospitali hizo.

Dkt. Shekalaghe amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa ambao umehusisha ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, hospitali za wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Rufaa za Kanda, kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa, ununuzi wa vifaa tiba na kuajiri watalaamu wenye weledi wa kada mbalimbali.

Dkt. Shekalaghe ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji huo ni wajibu wa watoa huduma kuanzia ngazi za chini mpaka Hospitali ya Taifa kuweka mikakati ya kutoa huduma bora na zinazokidhi matarajio ya wananchi kwa wakati kwa kutumia lugha yenye staha na unyenyekevu kitu kitakachowafanya waone matunda ya uwekezaji wa Serikali.

“Niwapongeze sana viongozi kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imekuwa ikijivunia huduma zenu, hizi hospitali ndio taswira ya taifa katika utoaji wa huduma hivyo ninyi mkifanya vibaya mnaharibu taswira ya nchi nzima” amesema Dkt. Shekalaghe

Pia, amewataka viongozi hao kuendelea kuzijengea uwezo Hospitali za Rufaa za Mikoa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa zina vifaa tiba, mashine za uchunguzi na wataalamu kitu kitakachosaidia kupunguza msongamano katika hospitali hizi na zenyewe ziweze kujikita katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amewashauri wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya pale wanapopewa maelekezo kwa kuwa wataalamu hao wana weledi wa kutosha na ushauri wao huwa unazingatia taratibu za kiafya.

Katika kikao hicho pamoja na Wakurugenzi wa taasisi hizo kimewashirikisha Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya Prof. Paschal Rugajo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili Prof. Appolinary Kamuhabwa.