SMZ KUWAWEZESHA VIJANA UJUZI NA VIFAA VITAKAVYOWASAIDIA KUPATA MIKOPO NA KUJIAJIRI

 

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Khalid Salum Mahammed.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawawezesha vijana kuwapa ujuzi na kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia kupata fursa ya mkopo na kujiajiri.

Dkt. Khalid amesema hayo, wakati akizungumza katika Mahafali ya 10 ya Chuo Cha Amali Mkokotoni,  yaliyofanyika katika chuo hicho Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa lengo la serikali kutoa ajira 300,000 kwa vijana Zanzibar.

Amesema, mafanikio mengi Duniani yanayopatikana yanatokana na mafunzo ya Amali hivyo ni vyema wahitimu hao kutumia fursa hiyo Kwa vitendo.

"Ili nchi iweze kufanikiwa ni lazima tupate watendaji wanaofundishwa katika vyuo vya Amali kwani itasaidia kupata Vijana wenye uweledi katika fani zao na Kuweza kuzifanyia kazi", amesema.

Aidha amewataka wahitimu hao kuanzisha vikundi na kuomba mikopo ili kuweza kuzitunza pesa zao kwa kufanya miradi itakayozalisha na sio kuzitumia fedha hizo bila malengo husika.

Amesema bila kuwa na ushirikiano w pande tatu kwa wanafunzi, wazazi na Waalimu,  hawawezi kufikia malengo ya kufanikiwa Katika masomo yao.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Vyuo vya Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Bakari Ali Silima, amesema kwa sasa mamlaka hiyo imeandaa darasa maalumu la kuwandaa wanafunzi ambao watakua na ujuzi zaidi ya mmoja, kuenda na soko la ajira liliopo.

Pia, amesema mamlaka ina ushirikiano na mashirika mbalimbali ambayo yanasaidia vyuo hivyo kwa kuwapatia vifaa pamoja na kuwapatia ujuzi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Vyuo na Mafunzo,  Mhandisi Abdalla Mohammed Hammbal, amesema fani mbali mbali zinafundishwa katika vyuo vya Amali zikiwemo, Umeme, Viyoyozi, ICT, hivyo Serikali inampango wa kuanzisha fani nyingine zinazoendana na Uchumi wa Blue  ili kuendana na Soko la Ajira kwa Vijana.

Akisoma risala kwa niaba ya  wanafunzi wa chuo hicho, Raya Salum Juma, wameiomba Serikali kuwapatia mikopo mikubwa ambayo itakayowasaidia kupata mitaji ya kuwasaidia kujiajiri kwa wasioajiriwa.

Raya amewaomba Vijana ambao wameshahitimu masomo yao kuwa na mtazamo wa kujiajiri kuliko kusubiri ajira kutoka Serikalini au kampuni binafsi.

Pia,  wameiomba Serikali ya Mkoa kuzungumza na wamiliki wa gari za abiria wapewe unafuu wa nauli kwa wanafunzi hao

Aidha, Waliiomba Serikali kujenga mabweni ya kutosha katika chuo chao ambayo yatachukua Wanafunzi wengi ili kuwasaidia Wanafunzi Wanaotoka Masafa ya mbali kwenda na kurudi.

Jumla ya Wanafunzi 259 wa fani mbali mbali Ikiwemo ICT, Kazi za Nyumbani,  Ufundi Umeme, Kilimo, wamehitimu na kupatiwa vyeti.